Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA INDIA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUENDELEZA TIBA ASILI, WHO YAPONGEZA


Na John Mapepele – New Delhi

Serikali ya Tanzania na India zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kuhusu ushirikiano kwenye Sekta ya Afya katika kuendeleza tiba asilia (Ayurveda), huku Tanzania ikiwakaribisha wawekezaji kutoka sehemu duniani kuja kuwekeza na kuwahakikishia kuwapatia mazingira mazuri ya uwekezaji.

Utiwaji saini huo kwa upande wa Serikali ya Tanzania umefanywa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Afya anayeshughulikia Tiba Asili (AYUSH) katika Serikali ya India Mhe. Jagat Prakash Nadda, kwenye Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu Tiba Asilia, uliomalizika hivi kwenye ukumbi wa kimataifa wa Bharat Mandapam jijini New Delhi India.


Aidha, utiwaji saini huo umeshuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ambapo ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa inayofanya kwenye sekta ya afya na kusisitiza kuwa WHO litaendelea kushirikiana kikamilifu.

Mhe. Mchengerwa amesema kusainiwa kwa hati hiyo ya makubaliano ni hatua muhimu kwa Tanzania, kwani kutaimarisha ushirikiano wa kitaasisi na India katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya afya, kuongeza uwezo wa rasilimali watu wa sekta ya afya, kuimarisha udhibiti na matumizi salama ya tiba asilia, pamoja na kuchangia jitihada za Serikali katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kufikia Bima ya Afya kwa Wote.

“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukuza tiba asilia salama, yenye ushahidi wa kisayansi na inayosimamiwa kwa misingi madhubuti ya udhibiti, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya afya kwa watu wote.” Amesisitiza Waziri Mchengerwa

Tanzania inaendelea kubadilisha tiba asili kutoka katika hekima ya kurithiwa kizazi hadi kizazi, na kuifanya kuwa tiba inayothibitishwa kisayansi, inalindwa kidijitali, na yenye uwezo wa kibiashara kwa manufaa ya afya duniani kote.

“Tunaamini kuwa tiba asilia, inapolindwa na Sheria, ikiimarishwa na Sayansi, ikiwezeshwa na Teknolojia, na kuendeshwa kwa mtazamo wa Kibiashara, inaweza kuwa nguzo muhimu ya kimataifa katika kujenga jamii zenye afya bora.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inaamini kuwa tiba asilia, inapolindwa na sheria, ikiimarishwa na sayansi, ikiwezeshwa na teknolojia, na kuendeshwa kwa mtazamo wa kibiashara, inaweza kuwa nguzo muhimu ya kimataifa katika kujenga jamii zenye afya bora.

Ameongeza kuwa tiba asilia bado ni muhimili muhimu wa HUDUMA ZA AFYA ya msingi nchini Tanzania, ambapo takribani asilimia 60 ya wananchi wetu hutumia huduma za waganga wa tiba asilia, ama kabla au sambamba na huduma za hospitali za kisasa ambapo amesema uhalisia huu unaonesha kuwa upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi si hiari bali ni jambo la lazima.
Ili kulilinda eneo hilo kisheria Mhe. Mchengerwa amesema TANZANIA imeweka msingi thabiti wa kisheria na kikanuni kupitia Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Na. 23 ya mwaka 2002, inayotekelezwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Aidha amesema Serikali inaendelea kuimarisha taasisi zinazohusika na tathmini ya usalama na ubora, zikiwemo TMDA, GCLA, NIMR na taasisi nyingine husika, lengo likiwa ni kuifanya tiba asilia iwe ya kitaalam kwa kulinganisha na viwango vya kimataifa vya ubora na usalama.

“Hatua inayofuata ni kuunganisha tiba asilia katika mfumo rasmio wa huduma za afya. Tanzania imejizatiti kuingiza tiba asilia katika huduma za afya ya msingi ili kuunga mkono lengo la Bima ya Afya Kwa Wote tangu mwaka 2023.” Amefafanua.


Pia amesema huduma za tiba asilia tayari zimeanza kutolewa katika hospitali rasmi, ambapo bidhaa 27 za tiba asili zilizothibitishwa zinatumika katika matibabu ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuanzisha mitaala ya kitaifa ya Tiba Asili, kutoa mafunzo kwa madaktari wa tiba ya kisasa na wataalamu wa tiba asilia, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Waganga wa Jadi na watoa huduma za afya ya kisasa ambapo baada ya kuunganishwa katika utoaji wa huduma za afya, tiba asilia pia itaakuwa chachu muhimu ya ubunifu na ukuaji wa uchumi.

Hadi sasa, bidhaa 141 za Tiba Asili zimesajiliwa nchini Tanzania, ambapo zaidi ya asilimia 90 huzalishwa na wajasiriamali wadogo wa ndani, kwa kuongozwa na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya.

Amesema ili kuwa na uendelevu Tanzania inakuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuimarisha kilimo cha mimea tiba, uchakataji na utengenezaji wa dawa, ubora wa uzalishaji, upatikanaji wa masoko na mauzo ya nje.

Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kukuza ushirikiano katika teknoloji, uhamishaji wa teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha bidhaa za tiba asilia za Tanzania zinakidhi viwango vya masoko ya kimataifa.

Pembezoni mwa mkutano huo Mhe. Mchengerwa amefanya majadilino na wawekezaji kadhaa wa sekta ya dawa lengo likiwa ni kuvutia uwekezaji wenye maslahi mapana kwa Tanzania.

Akifunga mkutano huo uliowashirikisha Mawaziri wa Afya kutoka zaidi ya nchi mia moja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, amesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki na maarifa ya jadi ya jamii, pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali kuhifadhi, kuthibitisha, na kulinda maarifa ya tiba asili. Vilevile, alieleza kuwa teknolojia haitachukua nafasi ya waganga wa jadi, bali itaongeza na kulinda hekima yao.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com