Na Mwandishi wetu, Arusha
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb.) ameipongeza Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kuendelea kuisimamia vyema Moduli ya Kupokea na Kushughulikia Malalamiko na Rufaa kieletroniki ambapo imekuwa nyenzo kwa wazabuni wenye malalamiko na rufaa.
Waziri Munde ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea Banda la PPAA pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) unaofanyika kwa siku mbili (tarehe 19 – 20 Desemba, 2025) Jijini Arusha.
Kadhalika, Mhe. Munde ameitaka PPAA kuendelea kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi hususan wazabuni ili waweze kuitumia Moduli hiyo kuwasilisha rufaa zao kwa wakati.
Nawapongeza PPAA kwa kuendelea kuisimamia vyema Moduli hii ya kuwasilisha malalamiko na rufaa……… endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mhe. Munde
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando, Mkuu wa Sehemu ya Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja PPAA imekuwa ikipokea rufaa kati ya 55 - 60 na zimekuwa zikishughulikiwa zote kwa wakati.
“Mhe. Naibu Waziri kupitia moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa ina faida kadhaa ikiwa ni pamoja kuokoa muda na grahama, imerahisisha upatikanaji wa nyaraka, kutunza kumbukumbu pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika michakato ya ununuzi na ugavi,” amesema Bi. Sayi
Aidha, Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi umewakutanisha wadau wa sekta ya ununuzi takribani 2,500 kutoka taasisi za umma na binafsi nchini pamoja na za nje ya nchi.
Mkutano huo umeongozwa na Kaulimbiu “Kujenga Wataalamu wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wa siku zijazo: “Uongozi na Ubunifu”.

Social Plugin