Ushindi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) nchini Eswatini si tukio la bahati, bali ni matokeo ya ujasiri wa Serikali kuachana na mifumo ya kizamani na kukumbatia teknolojia kama nyenzo ya kurejesha heshima ya mkulima.
Tukio hili linathibitisha kuwa Tanzania sasa imeamua kutumia akili ya kitafiti na uweledi wa hali ya juu wa wataalamu wake wa ndani kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Ufanisi huu umewezekana kutokana na usimamizi madhubuti wa Wizara ya Kilimo ambayo iliamua kuweka msukumo katika mifumo inayoziba mianya ya upotevu.
Serikali imekuwa ikisimamia kwa karibu uundaji wa Mfumo wa Kidijiti wa Pembejeo za Ruzuku, ikilenga kuhakikisha kuwa kila shilingi inayowekezwa kwenye kilimo inamfikia mlengwa halisi ambaye ni mkulima . Hatua hii imepunguza kwa kiasi kikubwa urasimu na udanganyifu uliokuwa ukijitokeza katika ugawaji wa mbolea nchini.
Kiwango cha utaalamu kilichoonyeshwa na TFRA katika mashindano hayo yaliyoshirikisha taasisi nyingi barani Afrika, ni uthibitisho kuwa vijana wa Kitanzania wana uwezo wa kubuni mifumo ya kidijiti inayoweza kushindana kimataifa.
Wataalamu wa TEHAMA ndani ya mamlaka hiyo wameonyesha uwezo mkubwa wa kutengeneza mifumo inayozungumza na mahitaji ya nchi, jambo ambalo limefanya mataifa mengine makubwa kama Afrika Kusini kutambua uwezo wa Tanzania. Maana yake ni kwamba Tanzania sasa inakuwa kitovu cha maarifa ya teknolojia ya kilimo barani Afrika, ambapo nchi nyingine zinaanza kugeuza macho huku ili kujifunza siri ya mafanikio haya.
Kwa mkulima wa Tanzania, mafanikio haya yana tafsiri ya moja kwa moja kwenye maisha yake ya kila siku. Mfumo huu wa kidijiti unampa mkulima uhakika wa kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei elekezi, bila kuingiliwa na watu wa kati wasio waaminifu. Hii ina maana kuwa ruzuku ya serikali sasa inafanya kazi iliyokusudiwa, ambayo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija shambani. Matokeo yake ni ongezeko la mavuno yanayopelekea usalama wa chakula na kuinua uchumi wa kaya za wakulima nchi nzima.
Ushindi huu pia ni ujumbe mzito kwa taasisi nyingine za umma. Kwa kuwa mfumo huu sasa umeanza kutumiwa na taasisi kama TOSCI, COPRA, na Bodi ya Korosho, ni wazi kuwa Tanzania inaelekea kwenye mfumo mmoja jumuishi wa kidijiti utakaorahisisha huduma zote za kilimo. Hii ndiyo maana halisi ya maendeleo; kutumia teknolojia kurahisisha maisha ya watu na kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya wengi, huku tukiandika historia mpya barani Afrika kama taifa la wabunifu na wazalishaji.

Social Plugin