
Agizo hilo, lililotolewa Desemba 29, 2025, wakati wa ziara ya kikazi katika kiwanda cha Pride of Nile wilayani Muleba, linapiga marufuku viwanda vya samaki kununua mazao moja kwa moja ziwani. Hatua hii si tu ya kiutawala, bali ni hitaji la kiuchumi linalolinda maisha ya maelfu ya Watanzania wanaotegemea maziwa yetu.
Hatua hii ya Balozi Dkt. Bashiru Kakurwa ni kielelezo cha uongozi unaotazama mbali. Inalenga kuondoa migongano ya kimaslahi kati ya wenye mitaji mikubwa (viwanda) na wavuvi wadogo, huku ikilinda mazingira. Ni wajibu wa mamlaka za mikoa na wilaya kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa ili kuokoa sekta ya uvuvi nchini.
Ukifanya uchambuzi wa hali ya sasa unaonesha kuwa ununuzi wa samaki moja kwa moja ziwani unaofanywa na viwanda umekuwa ukisababisha migongano mikubwa inayoua ajira kwa namna tatu.
Kushuka kwa Thamani ya Mvuvi Mdogo:
Viwanda vinapoingia ziwani, vinavunja mnyororo wa thamani. Mvuvi mdogo anakosa soko lenye ushindani na badala yake analazimika kuuza kwa bei ya chini inayopangwa na wenye viwanda, jambo linalomfanya ashindwe kujiendesha na hatimaye kuacha kazi hiyo.
Uchochezi wa Uvuvi Haramu:
Ununuzi holela majini umekuwa kichocheo cha uvuvi wa samaki wasioruhusiwa (wachanga). Hali hii inasababisha kupotea kwa mazalia, jambo ambalo kiwanda cha Pride of Nile kimekiri kuwa linashusha uzalishaji kutoka tani 20 hadi tani 3 pekee kwa siku. Uzalishaji unaposhuka, viwanda vinapunguza wafanyakazi na wavuvi wanakosa soko.
Biashara ya Mabondo na 'Wazazi':
Uwindaji wa samaki wakubwa (wazazi) kwa ajili ya mabondo pekee unaharibu mfumo wa ikolojia. Bila samaki wazazi, hakuna samaki wapya, na bila samaki wapya, hakuna ajira ya uvuvi kwa siku za usoni.
Umuhimu wa Marufuku ya Dkt. Bashiru
Marufuku ya Serikali imekuja kama "mkombozi" wa sekta ya uvuvi kutokana na Kurejesha nidhamu ya soko,kulinda mazalia ya samaki na kuongeza uzalishaji wa viwanda. Kwa kuwataka wenye viwanda kusubiri samaki nchi kavu, Serikali inatengeneza mfumo wa usimamizi (monitoring) ambapo samaki wanaovuliwa wanaweza kukaguliwa. Hii inahakikisha kuwa ni samaki halali pekee ndio wanaingia sokoni.Aidha kwa kupiga marufuku uvuvi wa samaki wazazi na biashara haramu ya mabondo ni kuhakikisha kuwa maziwa yetu yanabaki na utajiri wa kutosha. Hii inahakikisha kuwa ajira za wavuvi ni za kudumu na si za msimu.
Kama alivyobainisha mwakilishi wa kiwanda cha Pride of Nile, uvuvi haramu umepunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa. Marufuku hii ikitekelezwa, itasaidia samaki kuongezeka ziwani, viwanda vitapata malighafi ya kutosha, na hivyo kuongeza nafasi za ajira badala ya kuzipunguza.
Dkt. Bashiru ametoa onyo kali kuwa ni marufuku kwa kampuni yoyote isiyo na kiwanda kujihusisha na biashara ya mabondo. Huu ni mkakati wa kudhibiti utoroshaji wa rasilimali na kuhakikisha kila sehemu ya samaki inanufaisha uchumi wa ndani.
Social Plugin