Na Mwandishi wetu,Dodoma
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa shukrani kwa wananchi wote nchini kwa ushirikiano waliouonyesha katika kulinda na kudumisha amani kipindi chote cha Sikukuu ya Krismasi, iliyoadhimishwa 25 Desemba 2025.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Dodoma DCP David Misime
,amesema hatua hiyo imewezesha sherehe za mwaka huu kufanyika kwa utulivu na bila changamoto za kiusalama.
Amesema hali ya usalama imeendelea kuwa shwari katika maeneo yote ya nchi, huku wananchi wakiendelea kusherehekea sikukuu kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi bila wasiwasi wala hofu.
" Jeshi la Polisi limeeleza kuwa ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya ulinzi umekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha dhamira ya kulinda amani na kutengeneza mazingira mazuri ya kusherehekea, "amesema
Akitoa wito kwa umma, Msemaji wa Jeshi hilo amewataka Watanzania kuendelea kuilinda amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.
“Tunaendelea kuwasihi wananchi kudumisha amani kwani ndiyo inatupa fursa ya kusherehekea bila hofu tukiwa na marafiki na jamaa,” amesema.
Ameongeza kuwa bila amani hakuna shughuli za kijamii na kiuchumi zinazoendelea kwa ufanisi.
Kupitia taarifa hiyo amebainisha kuwa shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara, usafirishaji, huduma za kijamii na kazi za utumishi wa umma zinaendelea kama kawaida bila wasiwasi wowote.
Aidha Jeshi hilo linasisitiza wananchi kuendelea ushirikiano na utulivu huku likiahidi kuendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yo te na , kuhakikisha kila raia anabaki salama wakati wote.
Pia limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema pale wanapotilia shaka viashiria vya uvunjifu wa amani, ili kuchukua hatua za haraka na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.

Social Plugin