Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT HOMERA AKABIDHI MABOMBA YA SHILINGI MILIONI 30 KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA MAJI NAMTUMBO

Mwalimu Saidi Homera akikabidhi mabomba kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Zuberi Homera na Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania 

Na Mwandishi Wetu Malunde 1-Blog 

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amekabidhi mabomba yenye thamani ya shilingi milioni 30 kama hatua za dharura za kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo hilo. 

Msaada huo umetolewa kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji ya Serikali, ukiwa na lengo la kupunguza kero ya maji kwa wananchi wa Namtumbo.

Akikabidhi mabomba hayo kwa niaba ya Mbunge,  Mwalimu Saidi Homera amesema msaada huo umetokana na juhudi binafsi za Dkt. Homera, kama sehemu ya dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. 

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaonesha uwajibikaji na ukaribu wa mbunge kwa wananchi wake.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo, David Mkondya, amesema mabomba hayo yatatumika kukamilisha uchimbaji wa visima 10 katika vijiji 10. 

Baada ya uchimbaji, visima hivyo vitawekewa mifumo ya pampu za umeme na matenki ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 20,000 hadi 50,000 kulingana na idadi ya watu, hatua itakayoongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 74 hadi kufikia asilimia 76.

 Baadhi ya wakazi wa Namtumbo, akiwemo Diwani wa Kata ya Namtumbo Rajab Uhonde, wamempongeza na kumshukuru Dkt. Juma Homera kwa jitihada zake za kutatua changamoto za wananchi. 

Wamesema msaada huo unaonesha mbunge yupo karibu na wananchi na anashughulikia kero zao, huku wakimpongeza pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za Serikali katika ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika mji wa Namtumbo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com