Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI IKO MACHO: MBIBO AWATIA MOYO WATUMISHI OFISI YA RMO MARA



✅️ Asifu Kasi ya Makusanyo ya Maduhuli

✅️ Mara yafanikiwa kukusanya Tsh bilioni 112.61, sawa na asilimia 107.25 ya lengo la kipindi husika

✅️ Ahimiza Uzingatiaji Sheria, Taratibu na Misingi ya Utawala Bora

📍 Mara

Katika kuendeleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesisitiza kuwa Serikali iko macho na inaendelea kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika mazingira ya kazi ikiwemo kuendelea kuleta vitendea kazi vya kisasa ili kuboresha utendaji kazi wao na kutowakatisha tamaa.

Ameyasema hayo, leo tarehe 29 Desemba 2025 wakati akizungumza na watumishi wa Tume ya Madini Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Mara na kuwatia moyo watumishi hao kuwa Serikali inaendelea kuboresha changamoto ndogondogo zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Mbibo amewahakikishia watumishi hao kuwa Serikali ipo macho, inatambua changamoto zilizopo na tayari inaendelea kuzifanyia kazi hatua kwa hatua. Amesema uwepo wa vitendea kazi vipya, ikiwemo magari mapya, ni ushahidi wa dhahiri wa dhamira ya Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, Mbibo amewahimiza na kuwatia moyo watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwataka kuendeleza mshikamano, bidii na uvumilivu kazini, na kwamba changamoto hazipaswi kuwavunja moyo watumishi.

Sambamba na kukutana na watumishi hao kwa lengo la kuwasikiliza changamoto zao, Naibu Katibu Mkuu Mbibo pia amepata fursa ya kujionea kwa karibu mwenendo wa shughuli za kila siku, zinazotekelezwa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Mara.

Katika hatua nyingine, Mbibo ametoa pongezi kwa watumishi wa Ofisi hiyo kwa kazi nzuri ya makusanyo ya maduhuli inayoendelea kufanyika, akieleza kuwa matokeo hayo yanatokana na nidhamu, ushirikiano na uwajibikaji kazini na kuelekeza kuwa juhudi hizo ziendelezwe zaidi kwa kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya utawala bora.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Mara  Mhandisi Hamad Kallaye amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Mara umepangiwa lengo la kukusanya jumla ya shilingi bilioni 210.0. Hadi kufikia tarehe 28 Disemba, 2025, katika kipindi cha Julai hadi Disemba, Ofisi imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 112.61, sawa na asilimia 107.25 ya lengo la kipindi husika na asilimia 53.62 ya lengo la mwaka mzima.

Ziara hiyo imeacha taswira chanya miongoni mwa watumishi, ambao wameeleza kufarijika na kutiwa moyo na ujumbe wa Serikali, wakiahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo kwa maendeleo ya Sekta ya Madini katika Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com