Mwandishi wetu
Wanafunzi 40 walioteuliwa kuwa Mabalozi wa Uhifadhi na Utalii, wilayani Babati mkoa Manyara, wameahidi kuyalinda mapito ya wanyama(shoroba) ya kwakuchinja,yaliyopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge, iliyopo kati kati ya hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara kwa manufaa ya Taifa.
Wanafunzi hao kutoka shule nne za sekondari katika eneo la Burunge WMA, wametoa msimamo huo jana, baada ya kurejea katika ziara ya mafunzo ya Uhifadhi na Utalii, katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,mafunzo yaliyogharamiwa na Taasisi ya uhifadhi ya Chem Chem Assocition.
Kiongozi wa wanafunzi hao, Prosper Frank, ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mbughwe,wilayani Babati, alisema ziara yao ya mafunzo, wataitumia vizuri kutoa elimu katika jamii, kulinda mapito hayo ambayo yapo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara.
"Tumepata "madini" mengi kuhusiana na Umuhimu wa uhifadhi na Utalii na hivyo tumekuja na kauli mbiu yetu "Kwakuchinja corridor shall never die" ,tutatoa elimu shuleni, vijiji na tunaomba serikali iwe inatualika kwenye mikutano ili tutowe elimu ya uhifadhi na Utalii"alisema
Alisema wamekaa kwa siku nne katika hifadhi hiyo, sio kuona vivutio vya utalii pekee bali kila siku walikuwa na masomo juu ya uhifadhi, Utalii na Uzalendo kwa Taifa, jinsi ya kukabiliana na jinsi ya kupunguza migogoro baina ya binaadamu na wanyamapori bila madhara masomo ambayo yamewafungua kifikra na kuona wao kama vijana wanawajibu wa kulinda rasilimali za taifa kwa wivu mkubwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Babati,Afisa Tarafa hiyo, Emmiliana Fred alishukuru ChemChem kwa kuwezesha mafunzo kwa wanafunzi hao na kueleza serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji hao katika kukuza uhifadhi na Utalii nchini.
"Tumeelezwa hapa wanafunzi hao wamepatikana baada ya kufanya vizuri katika mitihani ya masuala ya uhifadhi na Utalii,Chem Chem mmefanya jambo kubwa sana na tunawapongeza kwani mmeeleza ziara hizi zitakuwa zinafanyika kila mwaka na tunaamini zitaongeza pia ufaulu wa wanafunzi wa sekondari mkoa wa Manyara"alisema
Alisema elimu ambayo wanafunzi hao, wameipata imewafanya kuwa mabalozi wa Utalii lakini pia itawasaidia hata kujiajiri katika masuala ya utalii na uhifadhi na hivyo,kujikwamua na umasikini badala kutegemea ajira za serikalini moja kwa moja.
"Sisi kama Serikali tutawashirikisha nyie wanafunzi kwenye shughuli za kiserikali, mje mtowe elimu, lakini pia tunataka mliojifunza yapelekeni shuleni, kwenye familia na katika jamii inayowazunguka"alisema
Mkurugenzi wa Chem Chem Association, Clever Zulu alisema, wanaamini mafunzo ya wanafunzi hayo yataleta mabadiliko makubwa ya kuendeleza uhifadhi na Utalii sio tu katika eneo la Burunge WMA wanapotoka bali kwa taifa zima.
"mafunzo hayo yamezalisha kina Nyerere wengine, wahifadhi, maprofesa na madaktari hivyo,tunatarajia baada ya mafunzo mtajiendeleza zaidi na kuwa mabalozi wazuri wa Uhifadhi na Utalii mkoa wa Manyara"alisema
Alisema taasisi ya Chem Chem ambayo imewekeza shughuli za utalii wa picha na hoteli katika eneo la Burunge WMA, itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha Burunge WMA inakuwa eneo la kipekee Afrika na hivyo kuendelea kuvutia maelfu ya watalii.
"Tunaipongeza pia serikali kwa kuendelea kutoa mazingira mazuri kwetu sisi wawekezaji na hadi sasa tumeamua kutoa kidogo tunachopata kwa mafunzo ya moja kwa moja kwa vijana katika kuendeleza uhifadhi na Utalii, lakini pia tulitoa basi la kupeleka watoto shule, tumesaidia miradi ya afya, maji ,Elimu na vikundi vya wanawake na vijana"alisema
Afisa Elimu Sekondari wa wilaya ya Babati,Akaro John ambaye pia aliambatana na wanafunzi hao, katika mafunzo akiwa na baadhi ya walimu, wazazi na viongozi wa vijiji, alisema wamejifunza mambo mengi na wanaamini yatasaidia utalii kwa wilaya ya Babati na mkoa wa Manyara.
"Ziara ilikuwa nzuri tulikuwa na wataalam wa Utalii na Uhifadhi,lakini pia wa masuala ya kijamii,tunaamini wanafunzi hawa watatumia vizuri elimu waliyopata ili kuendeleza utalii na Uhifadhi"alisema
Mkuu wa msafara wa wanafunzi hao, ambaye ni muongoza watalii kutoka kampuni ya Kananga alisema wamejitahidi kukaa vizuri na wanafunzi hao, kuwafundisha umuhimu wa uhifadhi na Utalii kwa uchumi wa Taifa na kikubwa kulinda mapito ya wanyama wa Kwakuchinja, kuondoa migogoro baina ya binaadamu na wanyamapori.
Akizungumza kwa niaba ya Wazazi wa wanafunzi hao, Dk Benson Andrea alipongeza Chem chem kwa kutoa mafunzo kwa watoto wao lakini pia kwa kazi nzuri wanayofanya kuendeleza uhifadhi na Utalii na kueleza jamii ya wananchi wa vijiji 10 ambao wanaishi katika eneo la Burunge WMA wataendelea kuwaunga mkono Chem chem katika kazi wanazofanya.







Social Plugin