Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UDSM YAISHUKURU SERIKALI YA AWAMU YA SITA KWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NA UTAFITI



Lindi — Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kukiimarisha kupitia uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na utafiti katika kampasi zake.

Shukrani hizo zimetolewa Jumamosi na Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Lindi ya UDSM.

Dkt. Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha elimu ya juu, katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025, ambapo Serikali itatekeleza miradi ya miundombinu ikiwemo ukarabati wa barabara katika maeneo ya Nane Nane (Ngongo) na ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita sita katika Kampasi za Ngongo na Ruangwa.

Miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya lami ya Kilambo (km 1.5), barabara ya Mtange–Kinengene–Kibaoni, pamoja na barabara ya Mahakama–Mitwero (km 1.2).

Akizungumzia Kampasi ya Kilimo ya UDSM mkoani Lindi, Dkt. Kikwete amesema ujenzi wake ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuifanya elimu ya juu kuwa nyenzo ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kampasi hiyo itazalisha wataalamu wa kilimo, utafiti na biashara ya kilimo, watakaosaidia kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kukuza ajira kwa vijana na kuinua kipato cha wakulima.

Ujenzi wa Kampasi ya Lindi unalenga pia kuimarisha tafiti bunifu zitakazochangia maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com