▪️Zaidi ya tani 100 - 120 kuchenjuliwa kwa siku
■ Makundi ya vijana na wanawake kupatiwa leseni kupitia programu ya MBT
■ Leseni zisizoendelezwa kufutwa kwa mujibu wa sheria
■ Aelekeza Wachimbaji kufuata kanuni za usalama za uchimbaji kuepuka madhara
https://www.malunde.com/2025/12/Mtambo-dhahabu.html
Mwakitolyo, Shinyanga
Kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwasimamia wachimbaji wadogo, Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ipo mbioni kuanza ujenzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya dhahabu mkoani Shinyanga.
Hayo yameelezwa leo tarehe 22 Desemba, 2025 na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi na kuzungumza na wachimbaji katika eneo la Mwakitolyo lililopo Shinyanga Vijijini.
Waziri Mavunde alitangaza habari hizo njema kuwa, tayari Shirika la STAMICO limeanza utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais na kwamba eneo limeshapatikana katika Kijiji cha Mawemelu na ujenzi utaanza hivi karibuni.
"Mhe. Rais aliona shughuli za uzalishaji mnazofanya hapa Mwakitolyo, akatuelekeza sisi Wizara kupitia STAMICO tulete mtambo wa Serikali hapa ili kuwezesha shughuli za uchenjuaji, mtambo ambao utakuwa na uwezo wa kuchenjua tani 100 hadi 120 za mawe kwa siku"
"Sambamba na hilo, tayari Serikali imenunua mitambo ya uchorongaji 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hii inaonesha nia thabiti ya Rais wetu Dkt. Samia ya kuwezesha shughuli za uchimbaji mdogo kufanyika pasipo kubahatisha" alisisitiza Mhe. Mavunde.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Sheria ya Madini Sura 123, Mhe. Mavunde alisema Kifungu cha 8 kimeweka zuio kwa Raia wa kigeni kuingia kwenye leseni za uchimbaji mdogo. Aidha, Kifungu cha 8 (3) kimeeleza iwapo ni muhimu, basi ni aina gani ya msaada wa kiufundi utolewe kwa wachimbaji wadogo na taratibu za kufuatwa, hili tunalisimamia ili kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo watanzania.

Aidha, Waziri Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kufuta leseni zote zisizoendelezwa kwa mujibu wa Sheria, kwani watu wengi wamekuwa wakihodhi maeneo na kuzuia fursa kwa wengine wenye uwezo na nia ya dhati ya kufanya shughuli za uchimbaji.
Maeneo hayo yatakayofutwa, tutayawekea mpango na kuyagawa kwenye vikundi vya vijana na wanawake ili wafanye uchimbaji ikiwa ni utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tommorow (MBT).
Awali, akieleza juu ya mipango ya Serikali kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse alisema mitambo 3 ya uchenjuaji ikiwemo miwili ya dhahabu Mwakitolyo na Buhemba, na mmoja wa Chumvi kujengwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kuhudumia wachimbaji wadogo.









Social Plugin