Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARAZA LA MADIWANI JIJI LA ARUSHA LAANZA RASMI, IRANQHE NA OLE SEKEYANI WACHAGULIWA KUONGOZA


Na Bora Mustafa, Arusha.

    Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanya mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani na kuwaapisha madiwani wa kata 25 pamoja na wajumbe 9 wa viti maalum.
 Zoezi la uapisho limefanyika chini ya hakimu mkazi mwandamizi, Boniface R. Semroki.

Aidha, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Mhe. Jacob Rombo, aliwapongeza madiwani wote waliochaguliwa kwa kuaminiwa na chama na wananchi. Pia alisisitiza wajibu wao katika kuendeleza maendeleo ya jiji.

Pia amesema kuwa katika kipindi ambacho madiwani hawakuwepo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, pamoja na watumishi wengine, waliendelea kutoa huduma kwa ufanisi. Hivyo, amewasihi madiwani kuendeleza pale walipoishia kwa kushirikiana na mkurugenzi.

Hata hivyo, mkutano huo uliambatana na uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Arusha. Mkurugenzi John Kayombo alisimamia upigaji kura ambapo jumla ya wapiga kura walikuwa 34, na wote wameshiriki.

Kwa upande wa Meya, Maxmillian Matle Iranqhe alikuwa mgombea pekee na alipata kura 33 za ndiyo na kura 1 ya hapana, hivyo akatangazwa mshindi rasmi. 

Aidha, kwa nafasi ya Naibu Meya, Julius Ole Sekeyani alipata kura 31 dhidi ya mpinzani wake Collince Nathan aliyepata kura 3.

Meya Maxmillian amewashukuru madiwani kwa imani waliyoonyesha kwa kumpigia kura, na pia akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake. Ameahidi kushirikiana na madiwani katika kuimarisha huduma za jamii kama barabara, utalii, elimu, na afya.

Aidha, amewahimiza watendaji wa kata kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka malalamiko au ufuatiliaji wa mara kwa mara kutoka kwa madiwani. Amesisitiza kuwa kazi ndio kipimo cha ufanisi wa utumishi wa umma.

Pia, ametangaza kuwa kikao hicho cha kwanza cha Baraza la Madiwani kinazindua rasmi kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa 2025–2030 kwa Jiji la Arusha.

Aidha, Mhe. Joseph Mkude ametoa pongezi kwa madiwani wote waliokula kiapo, na akamshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa kazi aliyoifanya kipindi chote ambacho madiwani hawakuwepo, akisema alihakikisha huduma kwa wananchi hazikukwama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com