
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahmudu Omary
Na Mbuke Shilagi, Kagera
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahmudu Omary, ameeleza sababu kuu zilizopelekea ushindi mkubwa wa chama hicho katika Uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Urais uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na mwandishi wetu leo Desemba 10, 2025, ofisini kwake, Hamimu amesema ushindi huo umetokana na ubora wa ilani za CCM, ubora wa wagombea, na mbinu za kisasa za kampeni zilizotumiwa na chama.
Amesema ilani ya CCM ya 2020–2025 pamoja na ya 2025–2030 zilikuwa msingi muhimu uliowezesha chama kupata ushindi wa kishindo, kwani ziliakisi mahitaji halisi ya wananchi na kutoa dira ya maendeleo.
Katibu huyo amebainisha kuwa uteuzi sahihi wa wagombea makini, waadilifu na wanaokubalika katika jamii uliwapa nguvu kubwa kwenye ushindani, na chama kilihakikisha kinaweka mbele watu wenye rekodi nzuri na wanaoaminika.
Amesema mbinu za kisasa zilizotumika, ikiwemo ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii, ubunifu katika kampeni, na matumizi ya teknolojia, ziliimarisha taswira ya chama na kuongeza imani ya wananchi.
“Kampeni zetu zilikuwa za kisasa, zenye ubunifu, na zilizojenga taswira mpya ya chama. Tulifanya kazi kama timu—wanachama, viongozi na wananchi,” amesema.
‘Kazi na Utu – Tunasonga Mbele’
Hamimu amesema kuwa kampeni za CCM zilitawaliwa na kutangaza kazi zilizokwishafanywa na Serikali ya Awamu ya 6 katika muhula wa kwanza, pamoja na kuahidi kufanya zaidi katika muhula wa pili.
“Tulikuwa tunatamba kwa kazi zilizokwisha kufanyika na tukijinadi kufanya zaidi kwa serikali hii hii ya Awamu ya Sita,” amesema.
Ameongeza kuwa CCM imeendelea kuimarisha utu, heshima, na umahiri katika kuhudumia wananchi bila ubaguzi.
Katibu huyo amesema kuwa chama kilijivunia kuendelea kulinda amani ya nchi, jambo ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa wapiga kura.
“Tunawalinda wananchi, tunawatumikia bila kujali rangi, dini au kabila. Amani yetu ndiyo hazina tuliyorithiwa na viongozi waliotutangulia,” amesema.
Ameongeza kuwa ushindi uliopatikana umetokana na umoja wa wanachama na wananchi kwa ujumla, ambao walifanya kazi kwa mshikamano na kujenga imani ya pamoja katika chama.
Social Plugin