Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KRISMASI NI SIKUKUU YA AMANI: MCHUNGAJI HANANJA NA WANANCHI WALAANI KUINGIZA UANAHARAKATI KWENYE IBADA

Kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja, ametoa wito mzito kwa Watanzania akisisitiza kuwa sikukuu hii ni mahususi kwa ajili ya kumtukuza Mungu na kuhubiri amani, na si jukwaa la harakati za kisiasa.

Mchungaji Hananja ameeleza kuwa jaribio lolote la kuingiza uanaharakati au maandamano ndani ya misingi ya kidini wakati wa msimu huu wa sikukuu ni sawa na kufuru. Akirejea maandiko matakatifu, amekumbusha kuwa ujumbe wa kwanza wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo ulikuwa ni amani kwa wanadamu.

"Krismasi ni sikukuu ya kumtukuza Mungu. Malaika walitangaza amani, na Luka 2:12 inatupa ishara ya mwokozi aliyeleta amani duniani. Kugeuza madhabahu au siku hii kuwa sehemu ya harakati ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu," alisema Mchungaji Hananja.

Kauli hiyo ya Mchungaji imeungwa mkono na sehemu kubwa ya wananchi ambao wamejitokeza kusisitiza umuhimu wa utulivu. Kupitia mijadala mbalimbali, wananchi wameonya dhidi ya vikundi vinavyojaribu kuchochea machafuko au maandamano wakati wa msimu wa sikukuu.

Wananchi wamehimiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na mshikamano wa kitaifa ni tunu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.

Kutokana na msimamo huo  wananchi wamekuwa mtandaoni  wakionesha msimamo dhidi ya maandamano kwa kauli mbiu za #Hatuandamani  huku wengi wakisema  kuwa wanaochochea vurugu wana ajenda za siri ambazo hazina maslahi kwa Taifa.

Wananchi wametoa tahadhari kwa vijana kutokubali kutumiwa na watu "waliohongwa" ili kuharibu utulivu wa nchi.

Mchungaji Hananja amewataka Watanzania kusherehekea kwa furaha na utulivu majumbani mwao na katika nyumba za ibada, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com