Kuelekea sherehe za Krismas na Mwaka Mpya, wananchi kutoka mikoa mbalimbali wametoa wito wa kutumia njia ya mazungumzo kutatua changamoto za kijamii badala ya kukimbilia vurugu ambazo zinahatarisha usalama wa taifa. Wito huo unakuja wakati Jeshi la Polisi likitangaza kuimarisha ulinzi kote nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani.
Edison Mhando, mkazi wa Songwe, amewataka Watanzania wenzake kuchagua amani na kuvumiliana, akisisitiza kuwa ulinzi wa amani ni jukumu la kila mwananchi na si la vyombo vya dola pekee. Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya polisi na jamii ni muhimu katika kudhibiti uhalifu, hasa baada ya uzoefu wa vurugu za huko nyuma zilizopelekea uharibifu wa mali za sekta binafsi ambazo ndizo kimbilio la ajira kwa vijana.
Jeshi la Polisi kupitia msemaji wao David Misime limetoa wito kwa wananchi wote kutambua thamani ya amani katika maisha yao na kuendelea kushirikiana na askari kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani.
Aidha, kutokana na kuongezeka kwa safari kipindi hiki, polisi wamewataka wasafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani kupitia kampeni ya “Endesha Salama, Familia inakusubiri” ili kuzuia ajali zinazoweza kuvuruga furaha ya sikukuu.
USHINDANI WA KIUCHUMI
Wakati Serikali ikielekeza nguvu zake katika kujenga uchumi wa uzalishaji na uongezaji thamani ili kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, wananchi wamesisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu itakayowezesha sekta binafsi kukua na kuchangia malengo hayo.
Aidha maoni haya yanakuja huku kukiwa na kumbukumbu ya hasara kubwa waliyopata baadhi ya wafanyabiashara Oktoba 29 kufuatia vurugu zilizosababisha uharibifu wa mali na makampuni kuchomwa moto.
Jackline Mwafongo, mkazi wa Mbeya, ameeleza kuwa bila amani, shughuli zote za kiuchumi, elimu, na maisha ya kawaida husimama. Amesema kuwa vurugu huleta hofu na uharibifu wa mali, jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za uwekezaji nchini. Kauli yake inaungwa mkono na Erick Emmanuel kutoka Dar es Salaam, aliyesisitiza kuwa vurugu husababisha hasara kubwa na maumivu kwa wananchi wasio na hatia, hivyo amani ni lazima ili kulinda ustawi wa shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, likibainisha kuwa utulivu huu ndio unaowezesha kila mmoja kushiriki katika shughuli halali za kiuchumi zinazopatia watu mahitaji yao ya kila siku. Jeshi limesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kukataa mipango yoyote inayolenga kuvuruga amani ili kulinda mnyororo wa uzalishaji na ajira zinazotolewa na sekta binafsi.
Social Plugin