Na Ahmed Salim Salim, Dar
Jumatano ya Oktoba 29, 2025, imeacha kumbukumbu chungu kwa Watanzania baada ya vurugu zilizojitokeza siku ya Uchaguzi Mkuu kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na shughuli za kiuchumi katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya ndiyo yaliyoathirika zaidi, sambamba na mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa ambako mali za umma na binafsi ziliteketea kwa moto.
Miongoni mwa waathirika ni kampuni ya Lake Oil Group, inayomilikiwa na Mtanzania mzawa, ambayo imepoteza vituo vyake 38 vya mafuta vilivyochomwa moto, hatua iliyosababisha zaidi ya wafanyakazi 300 kupoteza ajira zao.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Stephen Mtemi, amesema hasara iliyopatikana ni kubwa na imeathiri huduma za usambazaji mafuta nchini, huku akitoa pole kwa wananchi wote waliopoteza mali au kujeruhiwa katika matukio hayo.
Amesisitiza kuwa vurugu hazijawahi kuwa suluhisho la changamoto za kijamii au kisiasa, akiwataka Watanzania kudumisha amani na utulivu kama msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.




Social Plugin