
Na Deogratius Temba
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeendesha mafunzo maalumu kwa wajumbe wa Kamati za MTAKUWWA ngazi ya vijiji na kata katika Kata za Mamire (Babati DC) na Murray (Mbulu TC), yakilenga kuimarisha utendaji na kuongeza mbinu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Mafunzo haya ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na yanatekelezwa kupitia mradi wa Seedchange, unaolenga kuwawezesha wanawake wakulima vijijini kukuza ustahimilivu wa kiuchumi na kijamii.
Kupitia kilimo asilia cha ikolojia, wanawake wanasaidiwa kuongeza uzalishaji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha usalama wa chakula ngazi ya kaya, jambo linalochangia kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mafunzo yalijumuisha makundi mbalimbali muhimu katika jamii, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, watendaji, viongozi wa mila na dini, vikundi vya kijamii, asasi za kiraia, wakulima, wafugaji, na wazee maarufu.
Upana huu wa uwakilishi ulitoa fursa ya kujadili changamoto na majukumu ya kila kundi katika kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, sambamba na kuboresha mifumo ya utoaji taarifa na ulinzi kwenye jamii. Washiriki walisisitiza kuwa “kamati zetu zimeleta mabadiliko makubwa; watu wanaongeza uelewa na wanaripoti vitendo vya ukatili bila woga.”
Mafunzo haya pia yameshuhudiwa na maafisa mipango, maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kutoka halmashauri husika, ili kuhakikisha maarifa yaliyotolewa yanachangia upangaji wa bajeti zenye kuzingatia usawa wa kijinsia.
Uwepo wao umeongeza msukumo wa kutenga rasilimali za kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) 2023/24–2028/29 kwenye ngazi za halmashauri.
Mwakilishi wa Mkurugenzi kutoka Babati DC, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii (DCDO),January Bikuba alisisitiza: “Hatua hizi ni muhimu kuhakikisha bajeti inagusa maisha ya wanawake na watoto moja kwa moja. Tunawashukuru sana wadau wetu TGNP kwa jitihada, hizi na pia kuongeza maarifa kwa kamati zetu, tuna matumaini kabisa”
Mafunzo yamewezeshwa na Deogratius Koyanga kutoka TGNP, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uongozi, uwajibikaji na ushirikiano kati ya kamati na wadau wengine ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya ukatili. Washiriki kutoka Mamire na Murray wametoa ushuhuda wa mafanikio yaliyopatikana, wakibainisha kuongezeka kwa uwajibikaji wa jamii na hatua madhubuti zinazochukuliwa na kamati.






Social Plugin