Na Mwandishi wetu, Dar
Ghasia na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, jijini Dar es Salaam chini ya kivuli cha kile kilichoitwa “maandamano ya amani,” zimeacha athari kubwa za kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Tukio hilo limepelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umma ikiwemo ofisi za Serikali za mitaa, vituo vya mafuta, magari binafsi na ya umma, pamoja na vituo vya mwendo kasi vilivyoteketezwa kwa moto.
Watu waliokuwa wakijitokeza kudai haki zao waligeuza maandamano hayo kuwa machafuko yaliyoleta taharuki na hasara kwa wananchi wengi.
Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa vurugu hizo ziliibuka ghafla na kuenea katika mitaa kadhaa ya jiji, hali iliyosababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama kwa muda. Wafanyabiashara, madereva na wakazi wa maeneo yaliyoathirika wamelalamikia hasara kubwa waliyoipata, wakitoa wito wa kulindwa kwa amani na mali za wananchi.
Serikali imesisitiza kuwa itachukua hatua kali dhidi ya wale wote waliotumia maandamano hayo kufanya uhalifu na kuharibu mali za umma, huku ikitoa wito kwa wananchi kuendelea kutafuta haki kwa njia halali na za kistaarabu.




Social Plugin