Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAFARI YA UTHUBUTU: MASHINDANO YA QUR’AN KWA WENYE ULEMAVU YAZINDULIWA




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Katika hatua inayofungua ukurasa mpya wa historia, jiji la Dodoma limezindua msimu wa pili wa Mashindano ya Kusoma Qur’an Tukufu kwa Watu Wenye Ulemavu tukio ambalo limeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuandaa mashindano ya aina hii kwa kiwango cha kitaifa.

Uzinduzi huo umeakisi dhana ya ushirikishwaji, heshima na kuibua vipaji, sambamba na kuthibitisha kuwa ulemavu si kikwazo cha imani, elimu wala uwezo.

Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Ummy Ndeliananga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuipa nguvu kubwa agenda ya ustawi wa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuhakikisha wanapata fursa, utu na nafasi sawa kama wananchi wengine.

Amesema hatua hizo zimeondoa woga, kuleta tabasamu na kuongeza imani ya kundi hilo kushiriki katika shughuli za kijamii na kitaifa.

Naye Mwanzilishi wa mashindano hayo na Mkurugenzi wa Riziki Rurida Foundation, Riziki Saidi Rurida, amesema wazo la kuanzisha mashindano lilitokana na uzoefu alioupata kupitia mikutano ya kimataifa ya watu wenye ulemavu pamoja na huduma za kipekee alizopata wakati wa hija mjini Makka.

Amesema ulemavu wake ulisababishwa na ajali, lakini hakuruhusu hali hiyo iwe kikwazo cha kuchochea mabadiliko.

Kwa mwaka wa kwanza wa mashindano, baadhi ya washindi waliwezeshwa pikipiki na bajaji kama hamasa ya kujitegemea kitu ambacho amesema kimeongeza morali kubwa mwaka huu.

Amesisitiza kuwa leo watu wenye ulemavu wana miundombinu yao, wanaheshimiwa na hawanyanyapaliwi kama ilivyokuwa zamani.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuacha ubaguzi katika ndoa, akisema upendo ndio msingi wa baraka na hata kiimani kitendo hicho kina thawabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amesema mashindano hayo yanawaunganisha watu wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali na kuwawezesha kuonesha vipaji vyao kwa ujasiri.

Amesema matarajio makubwa ni kuyaona mashindano yakifika ngazi ya kimataifa, na ametoa wito kwa wenye ulemavu wote kujitokeza kwa wingi kwa kuwa fursa zimeongezeka na zawadi zimeboreshwa.

Mwakilishi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu mkoani Dodoma, Hussein Ramadan Ngula, amesema msimu huu umeongeza imani kuwa watu wenye ulemavu wanathaminiwa kama wengine, na kwamba maamuzi ya pamoja yanayomtegemea Mungu bila kubaguana ndiyo msingi wa jamii inayojenga utu na usawa.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Hidaya Abdallah, amesema mashindano haya yanaongeza uelewa wa Qur’an, kuimarisha usomaji na kujenga jamii inayotambua haki za watu wenye ulemavu na kwamba umuhimu wake unapaswa kufikishwa kwa makundi yote ya rika ili taifa liendelee kujisuka kwa misingi ya ushirikishwaji.

Ikiwa ni msimu wa pili tu, mashindano haya yameibua matumaini, yamejenga hadhi mpya na yameonesha kwa vitendo kuwa vipaji havizuiliwi na hali ya mtu.

Ikiwa yatafika ngazi ya kimataifa kama ilivyopendekezwa, Tanzania itazidi kuandika historia katika kuunganisha imani, vipaji na ujumuishi kwa manufaa ya watu wote.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com