Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi,akizungumza na maafisa usafirishaji wa kijiwe cha Mchongamani Wilayani humo walipokuwa kwenye hafla ya kula na kunywa ikiwa ni sehemu ya kuimarishana kiuchumi na kijamii Novemba 23,2025 katika viwanja vya Storm palace hotel
Na Sumai Salum – Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amepongeza Umoja wa maafisa usafirishaji (Bodaboda)wa Kijiwe cha Mchongomani kwa kufanikisha mkutano wa pamoja wa kijamii uliolenga kujenga mshikamano, kusikilizana na kujadili changamoto zinazowakabili katika kazi zao za kila siku.
Tukio hilo limefanyika Novemba 23, 2025 katika uwanja wa Hoteli ya Storm Palace, iliyoko mtaa wa Mhunze ya Juu, ambapo waendesha bodaboda wamekutana kula, kunywa na kufurahi pamoja kama sehemu ya kuimarisha umoja na afya ya kijamii ndani ya kundi hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masindi ameuita mkutano huo kuwa ni hatua yenye afya na chachu ya maendeleo kwa vijana hao, akisema kuwa umoja huo unajenga nidhamu, ushirikiano na hamasa ya kufanya kazi kwa uadilifu.
Amesema vijana hao wamekuwa mfano bora wa kuigwa kwani mbali na kujumuika kwa furaha, wameonesha uzalendo kwa kulitakia Taifa amani, wakitambua kuwa sekta ya usafirishaji ndiyo mhimili wanaoutegemea katika kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine, hafla hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wafanyabiashara kutoka maeneo tofauti wilayani Kishapu, jambo lililowapa fursa za kujadiliana namna ya kuboresha huduma za usafirishaji na kuongeza tija katika shughuli zao, huku akishiriki kuwachangia Tsh.600,000 kwa kushirikiana na wadau wengine kwa lengo la kukuza mfuko wao.
Kauli ya Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji
“Tuliamua kukaa pamoja, kula na kufurahi kama familia moja kwa sababu tunatambua nguvu ya umoja. Hii ni nafasi ya kujengeana, kusikilizana na kutiana moyo katika kazi zetu. Tumefurahi kuwa pamoja, na tutafanya hivi mara kwa mara kwa ajili ya maendeleo yetu,” amesema.
Social Plugin