
Mussa Azzan Zungu
Na Dotto Kwilasa - Malunde 1 blog Dodoma
Aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge lililopita na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu, amechaguliwa kwa kishindo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi huo wa ndani ya chama umefanyika leo Novemba 9, 2025 jijini Dodoma, na umehudhuriwa na wabunge wa CCM kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika matokeo hayo, Zungu ameibuka na ushindi mkubwa baada ya kupata kura 348, akimshinda mpinzani wake pekee, Stephen Masele, aliyepata kura 16.
Zungu, ambaye ni amezaliwa wa mwaka 1952, sasa ndiye Spika mtarajiwa wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia hatua ya aliyekuwa mgombea, Dkt. Tulia Ackson, kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho mapema wiki hii.
Kwa upande wa nafasi ya Naibu Spika, Mbunge Daniel Silo ameibuka kidedea kwa kupata kura 362, huku wagombea wengine waliokuwa wamejitokeza awali wakijiondoa kabla ya upigaji kura kuanza. Kura mbili ziliharibika.
Uchaguzi huu wa ndani ya CCM ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi rasmi wa Spika na Naibu Spika utakaofanyika ndani ya Bunge, ambapo chama tawala kinatarajiwa kuendelea kushikilia nafasi hizo kutokana na wingi wa wabunge wake.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema ushindi wa Zungu unadhihirisha umoja na msimamo wa wabunge wa CCM katika kuhakikisha uongozi wa Bunge unaendelea kuwa thabiti, wenye uzoefu na uadilifu.

Social Plugin