Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YATHIBITISHA USHIRIKI WAKE COP30: YAJIPANGA KUONGOZA SAUTI YA AFRIKA DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI

Na Kadama Malunde

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitisha ushiriki wake katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), unaotarajiwa kufanyika Novemba 10 hadi 21, 2025, jijini Belém, Brazil.

Tanzania, ikiwa ni mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris, itaungana na mataifa mengine duniani kujadili njia za kuharakisha utekelezaji wa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Cyprian Luhemeja, amesema mkutano wa COP30 hautakuwa tu jukwaa la majadiliano ya kisera, bali pia ni fursa muhimu kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo duniani katika juhudi za kuhamasisha rasilimali fedha, teknolojia bunifu na uwekezaji wa kijani unaolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

COP30 siyo tu mkutano wa majadiliano, bali ni jukwaa la kimataifa linalotupa nafasi ya kuongeza ushirikiano na wadau duniani kote kwa lengo la kukuza uchumi wa kijani, kuimarisha maendeleo endelevu na kulinda vizazi vya sasa na vijavyo dhidi ya athari za tabianchi,” amesema Luhemeja.

Luhemeja amefafanua kuwa Tanzania imezindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, inayolenga kujenga taifa lenye ustawi jumuishi, uchumi shindani wa kijani na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, kwa kuhusisha sekta zote za maendeleo katika utekelezaji wake.

Aidha, Serikali imeanza maandalizi ya nyenzo mahsusi za utekelezaji wa dira hiyo, sambamba na kukamilisha michango iliyosasishwa ya kitaifa (NDCs) na mipango ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 
"Hatua hizi zimeweka Tanzania katika nafasi bora ya kuwasilisha matokeo halisi na mpango kazi thabiti kwenye mkutano wa COP30 nchini Brazil", ameeleza.

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Dkt. Richard Muyungi, amesema mkutano wa COP30 utakuwa ni jukwaa muhimu kwa bara la Afrika kuendeleza ajenda yake ya haki ya tabianchi, usawa wa kijinsia, nishati safi na ushiriki wa vijana katika mabadiliko ya tabianchi.

Afrika lazima iakisi hali halisi ya jamii zake, hasa wanawake na vijana wanaokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa nishati safi na ajira rafiki kwa mazingira. Tanzania, ikiwa kinara wa kundi la AGN, ina wajibu wa kuhakikisha sauti za bara letu zinasikika na kuzingatiwa katika maamuzi ya kimataifa,” amesema Dkt. Muyungi.

Kwa mujibu wa kauli mbiu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “Dira 2050: Utekelezaji wa Hatua Jumuishi za Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi”, nchi inalenga kuhakikisha maendeleo ya kijani na ustahimilivu wa mazingira yanakuwa sehemu ya ajenda kuu ya kitaifa.

Tanzania, ikiwa Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), itatumia nafasi hiyo kuongoza sauti za bara la Afrika katika kupigania upatikanaji wa fedha, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa utakaosaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na changamoto hizo.

Ushiriki wa Tanzania katika COP30 unathibitisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa sehemu ya jitihada za kimataifa za kulinda mazingira, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kujenga uchumi wa kijani unaozingatia ustahimilivu, ushirikishwaji na maendeleo endelevu.


Tanzania inabaki kuwa mstari wa mbele katika kulinda sayari yetu, kuhimiza usawa wa tabianchi na kuhakikisha maendeleo ya kijani yanakuwa urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com