Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MISIME: UANDISHI WA AMANI NI NGUZO YA UMOJA NA UTULIVU NCHINI


Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP David Misime

Na Kadama Malunde – Dodoma

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP David Misime, ametoa rai nzito kwa vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinaandika na kuripoti taarifa sahihi, zilizohakikiwa na zisizo na mwelekeo wa uchochezi, ili kulinda amani, umoja na utulivu wa taifa.

Akizungumza leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma katika mafunzo ya Uandishi wa Habari za Amani yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA-TAN), DCP Misime amesema kumekuwa na ongezeko la taarifa zisizo na uthibitisho kusambazwa hasa kupitia mitandao ya kijamii, hali inayoweza kusababisha taharuki na kuhatarisha usalama wa nchi.

“Wajibu wa chombo cha habari ni kuelimisha, kuhabarisha na kujenga jamii, badala ya kusambaza taarifa zinazoibua hofu isiyo ya lazima,” amesema Misime, akibainisha kuwa taarifa nyingi zisizo sahihi zimekuwa zikitumiwa vibaya na watu wenye nia ya kupotosha au kutoa msukumo wa migogoro.

Akitolea mfano mwenendo wa baadhi ya vyombo vya habari vya mtandaoni, Misime alisema kumekuwa na tabia ya kipaumbele kutafuta “views” kuliko kutoa taarifa za kuaminika, jambo ambalo alisema linaweza kuchangia kuporomoka kwa ustawi na usalama wa nchi.

“Katika habari za amani, nawaomba waandishi muepuke taarifa zinazochochea chuki na kuhatarisha nchi. Toeni taarifa sahihi, zilizothibitishwa na mamlaka husika, na msiegemee upande mmoja hata pale zinapotokana na matamko ya kisiasa,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kufanya uchambuzi wa kina, uhakiki wa taarifa na kufuata maadili ya taaluma kabla ya kuchapisha au kurusha habari, sambamba na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za serikali ili kupunguza mkanganyiko kwa wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na taarifa wanazosambaza, akisema kila mtu anapaswa kuchangia katika kulinda amani na utulivu wa taifa kupitia matumizi sahihi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuandika taarifa za kuhamasisha amani, kupunguza lugha za chuki, kuchambua habari zenye dalili za upotoshaji na kuimarisha uzalendo na mshikamano wa taifa.

Kwa mujibu wa Soko, mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha vyombo vya habari vinaendelea kuwa nguzo ya kudumisha amani nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho taarifa za uchochezi na za kupotosha zimekuwa zikisambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com