Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAHANATI MPYA YA KIJIJI CHA LUGALI YAMALIZA MATESO YA WANANCHI YAWAPUNGUZIA SAFARI ZA MATIBABU

Mganga wa zahanati ya Lugali Theodora Lusendamila akiwa anamuhudumia mgonjwa aliyekuja kutibiwa katika zahanati hiyo 

Na Regina Ndumbaro- Mbinga

Wananchi wa Kijiji cha Lugali, Kata ya Mkumbi, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati yao, hatua iliyowapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. 

Wamesema ujenzi wa zahanati hiyo umeleta unafuu mkubwa, hasa kwa akina mama wajawazito na watoto waliokuwa wakiteseka kwa safari ndefu kwenda kituo cha afya Mkumbi au Hospitali ya Wilaya mjini Mbinga.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Lucy Ndunguru amesema zahanati hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii yao kwani sasa wanapata huduma karibu na makazi yao, jambo linalowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kama kilimo. 

Naye Fidea Kapinga ameeleza kuwa kabla ya zahanati kufunguliwa walilazimika kutembea zaidi ya kilomita tatu kufuata matibabu, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wajawazito na watoto.

Mganga wa zahanati hiyo, Theodora Lusendamila, amewapongeza wananchi kwa kujitolea nguvu kazi hadi kukamilika kwa ujenzi huo, akibainisha kuwa huduma zinazotolewa sasa zimemaliza kabisa changamoto ya huduma za afya iliyokuwepo kwa muda mrefu. 

Amesema magonjwa yanayoongoza kutibiwa katika zahanati hiyo ni ya ngozi (hasa kwa watoto), nimonia na malaria, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata matibabu badala ya kutumia dawa za asili zisizothibitishwa.

Kwa upande wake, katibu wa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga George Mhina, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma katika zahanati hiyo kwa kupeleka dawa na vifaa tiba vya kutosha. 

Amesisitiza kuwa tangu zahanati ilipoanza kutoa huduma rasmi mwezi februari mwaka huu imeleta faraja kubwa si kwa wananchi wa Lugali pekee bali pia kwa vijiji jirani na kuwataka wananchi waendelee kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassa



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com