Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wazee wa mkoa huu kutumia nafasi yao kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, sambamba na kuwasihi vijana kudumisha amani ya nchi.
Akizungumza na wazee hao Oktoba 9 , 2025 jijini hapa Senyamule amesema wazee wana mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.
“Ni jukumu la kila mwananchi kuchagua viongozi wenye tija na maendeleo,Wazee mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi, kwani maendeleo yaliyofanywa na Serikali yanaonekana wazi,” amesema Senyamule.
Ameongeza kuwa Dodoma ya sasa ni tofauti na ile ya miaka 10 iliyopita kutokana na kasi ya maendeleo, uboreshaji wa miundombinu na ongezeko la fursa za uwekezaji.
“Dodoma ya sasa inavutia na imekuwa kimbilio la Watanzania na wageni wa kimataifa,Mabadiliko haya ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kulinda amani,” ameongeza.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amesema Serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa kwa wazee ili kuboresha afya zao kupitia mazoezi na lishe bora kulingana na umri.
“Kupitia nyie wazee, Serikali itaweza kubaini changamoto zenu na kuhakikisha zinatatuliwa, kwani wazee ni tunu ya taifa hili,” amesema.




Social Plugin