Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE RUVUMA WAFANYA MAOMBI MAALUM KUOMBEA UCHAGUZI WAZIRI WA AFYA JENISTA MHAGAMA ATOA WITO WA AMANI NA USHIRIKI KATIKA UCHAGUZI

Waziri wa Afya Jenista Mhagama akiwa anazungumza na wanawake Mkoani Ruvuma waliojitokeza kwenye maombi maalum ya kuliombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu leo katika ukumbi wa Songea Club Manispaa ya Songea 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Wanawake mkoani Ruvuma leo Oktoba 26, 2025, wamefanya maombi maalum katika Manispaa ya Songea kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu maombi hayo yakiwa na lengo la kuliombea Taifa liwe na uchaguzi wa amani, utulivu na maendeleo. 

Tukio hilo limewakutanisha  kwa pamoja  waumini wanawake na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ikiwemo BAKWATA, TEC, CCT, CPCT, KKKT, Mashahidi wa Yehova na Wasabato, wote wakishirikiana kumuomba Mungu aijalie Tanzania uchaguzi salama na wenye kumpa ushindi kiongozi mwenye maono ya maendeleo.

Mgeni rasmi katika maombi hayo ni Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, ambaye amewataka wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wenye sera bora zitakazoboresha huduma muhimu kama afya, kilimo na uchumi. 

Amesema wanawake wanayo nafasi kubwa katika kulinda amani na kuleta maendeleo kwa kuwa ni nguzo muhimu katika jamii na familia.

Mhagama amesisitiza umuhimu wa maombi hayo akisema yana nafasi ya kipekee katika kumuomba Mungu awape wanawake hekima na uwezo wa kutambua viongozi wenye nia njema ya kulitumikia Taifa. 

Ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kuwa mabalozi wa amani katika kipindi hiki cha uchaguzi, wakikataa kugawanywa kwa misingi ya dini, kabila au itikadi za kisiasa. 

“Ni jukumu letu kuhakikisha amani inatawala katika Mkoa wa Ruvuma na nchi yetu kwa ujumla,” amesisitiza Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza misingi ya amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa licha ya changamoto zilizokuwepo baada ya kupokea uongozi kutoka kwa mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. 

Amesema uongozi wa Dkt. Samia umeendelea kujikita katika kuimarisha ustawi wa wananchi na kukuza maendeleo ya Taifa.

Mhagama amesema kuwa wananchi wote waliofikisha umri wa miaka 18 kuhakikisha wanatumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025, ili kuwachagua viongozi watakaoliletea Taifa maendeleo chanya. 

Maombi hayo yamefungwa kwa sala za pamoja za kuombea uchaguzi, viongozi wa nchi na ustawi wa Taifa la Tanzania.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com