Na Mwandishi wetu, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, ametoa onyo kali kwa makundi au watu wenye nia ya kuanzisha vurugu wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na makini kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini.
Kauli hii imetolewa leo, Jumatano Oktoba 22, 2025, wakati wa Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu, lililoandaliwa na Taasisi ya Ukumbusho wa Zakkat Tanzania na kufanyika mkoani Morogoro.
Mhe. Malima alibainisha kuwa baadhi ya watu wanaojaribu kuvuruga amani nchini ni wale wanaoshawishiwa na matendo kutoka nje na hawana nia njema kwa Taifa.
Akizungumza pia katika kongamano hilo, Sheikh Alhad Mussa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), aliwaasa Watanzania kukataa kwa nguvu zote watu wanaoeneza chuki na kuhatarisha maisha ya wengine, hasa katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi.
Aidha, Dkt. George Pindua, Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, aliahidi kuwa viongozi wa dini wataendelea kuhubiri amani, mshikamano na upendo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Onyo la RC Malima linatuma ujumbe thabiti: vyombo vya usalama vipo makini, na hakuna mtu atakayekubaliwa kuvuruga amani. Wote wanaopanga au kuratibu fujo watakabiliana na sheria, huku wananchi wakihimizwa kushirikiana kuhakikisha uchaguzi unaenda kwa amani.



Social Plugin