Jamii ya Wahadzabe wanaoishi eneo la Mang’ola, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wameelezea furaha na hamasa yao kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ijayo, Oktoba 29, 2025, wakiahidi kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya Kikatiba ya kupiga kura.
Wakizungumza leo Jumatano, Oktoba 22, 2025, wananchi hao wamesema wanajivunia kuhusishwa katika mchakato wa uchaguzi licha ya kuishi maeneo ya pembezoni, wakieleza kuwa hatua hiyo inaonesha serikali imewakumbuka na kuwathamini kama Watanzania wengine.
“Kwaniaba ya wenzangu Jamii ya Wahadzabe, niwahakikishie kuwa tutaenda kupiga kura tarehe 29 na tutachagua viongozi watakaotuangalia sisi wote kwa ujumla ili tufanikiwe kimaendeleo.
Tunaishi porini, hatujui mengi yanayoendelea, hivyo tunataka viongozi watakaotuletea maendeleo huku,” amesema mmoja wa wazee wa jamii hiyo.
Kwa upande wao, Ruben Mathayo, Mwenyekiti wa Jamii ya Wahadzabe Tanzania, na Mariam Anyanyire, Mhamasishaji wa ndani ya jamii hiyo, wamesema kuwa muamko wa wananchi ni mkubwa na maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea siku ya kupiga kura.
“Wahadzabe tumejipanga, kila mwenye haki na sifa ya kupiga kura atashiriki. Tunatambua umuhimu wa uchaguzi huu kwa mustakabali wa maendeleo ya jamii yetu,” amesema Mathayo.
Wameongeza kuwa jamii hiyo imepata elimu ya uraia kupitia viongozi wa serikali na mashirika mbalimbali, jambo lililosaidia kuongeza uelewa wa umuhimu wa kushiriki kwenye chaguzi za kidemokrasia.
Jamii ya Wahadzabe ni miongoni mwa jamii za asili nchini Tanzania, maarufu kwa mfumo wao wa maisha wa uwindaji na ukusanyaji wa matunda, na imekuwa ikiendelea kuunganishwa na mifumo ya kisasa ya kijamii kupitia juhudi za serikali na wadau wa maendeleo.




Social Plugin