Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUME YA UCHAGUZI YAONYA: KUSHAWISHI WATU WASIPIGE KURA NI KOSA KISHERIA



Na mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima, ametoa onyo kali kwa watu au makundi yanayohamasisha wananchi kutoshiriki kupiga kura, akisema kitendo hicho ni kosa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha UTV, Kailima amesema kifungu cha 129 cha sheria hiyo kinaeleza wazi kuwa mtu yeyote anayetumia nguvu, vitisho au udanganyifu kumshawishi mpiga kura kuacha kupiga kura anatenda kosa la ushawishi mbaya, na anaweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Amefafanua kuwa kifungu hicho kinakataza mtu yeyote kutumia au kutishia kutumia nguvu, vurugu, au hila ya aina yoyote kwa lengo la kumshawishi mpiga kura kupiga au kuacha kupiga kura, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kuvunja masharti hayo.

Aidha, Mkurugenzi huyo amewakumbusha wananchi kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba, na kushiriki katika uchaguzi ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya nchi na kuimarisha demokrasia.

“Tume inawahimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi kwa amani, utulivu na kufuata sheria za nchi,” alisisitiza Kailima.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, ambapo Watanzania watapiga kura kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani katika maeneo yote nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com