Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TTCL YASISITIZA KUWA KARIBU NA WATEJA WAKE




Na Mwandishi Wetu,

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limedhamiria kuendelea kutoa huduma bora na za kuaminika kwa wateja wake kote nchini, likisisitiza kuwa litasikiliza maoni ya wateja wake kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kila mmoja anapata thamani anayostahili.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Humphrey Ngowi, alisema shirika hilo limejipanga kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuwa bora zaidi kwa kutumia teknolojia za kisasa na kwa kuzingatia mrejesho kutoka kwa wateja.

"Wiki hii imetuwezesha kutathmini mafanikio yetu, kubaini maeneo ya kuboresha, na kujifunza mbinu mpya za kuboresha huduma zetu kwa wateja," alisema Ngowi.

Ngowi alibainisha kuwa TTCL, kama taasisi kongwe ya mawasiliano nchini, imeendelea kuwa kiunganishi muhimu kwa Watanzania wa mijini na vijijini, hasa katika kipindi hiki ambapo dunia inabadilika kwa kasi kubwa kiteknolojia.

Alisema kuwa kupitia kauli mbiu ya mwaka huu ya "Mission Possible", TTCL imefanikiwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kujenga mshikamano baina ya wafanyakazi na wateja wake.

"Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa la wazi kwa wateja kutoa maoni yao, na sisi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuimarisha huduma zetu. Tumepokea mrejesho mzuri ambao sasa unatuongoza kwenye maboresho ya kimkakati," aliongeza.

Katika hatua nyingine, Ngowi alisema kuwa TTCL imeendelea kutekeleza miradi ya kupanua huduma katika maeneo ya mijini na vijijini, sambamba na kuimarisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na ujenzi wa minara mipya ili kuongeza upatikanaji wa huduma hata katika maeneo yaliyo pembezoni.



Wiki ya Huduma kwa Wateja ilianza rasmi Oktoba 6 na kufikia kilele chake Oktoba 10, ambapo TTCL ilitumia nafasi hiyo kuonyesha dhamira yake ya kuendelea kuwa karibu na wateja wake na kuthibitisha kuwa "Mission Possible" siyo tu kauli mbiu, bali ni njia ya maisha ndani ya shirika hilo.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com