Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANESCO MKOA WA SHINYANGA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA KUKUTANA NA WATEJA WAKUBWA

Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga limefanya kikao maalum na wateja wake wakubwa, kikao ambacho kimefanyika kwa mafanikio makubwa na kuonesha dhamira ya dhati ya shirika katika kuimarisha mahusiano bora na wateja wake.

Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Meneja wa Mkoa, Mhandisi Seraphine Lymo, ambaye ametoa shukrani za dhati kwa wateja kwa kuendelea kushirikiana na TANESCO kwa karibu, kuwa bega kwa bega na shirika, na kuwekeza kwa njia chanya katika maendeleo ya sekta ya umeme mkoani Shinyanga.

Amesisitiza kuwa TANESCO itaendelea kuboresha huduma zake, kuongeza ufanisi katika utoaji wa umeme wa uhakika, na kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, za haraka na zenye ubora wa hali ya juu.

"TANESCO inaendelea kuwashukuru wateja wake wote kwa ushirikiano, uaminifu na maoni yao yenye kujenga. Shirika linaahidi kuendelea kuboresha huduma, kusikiliza maoni ya wateja, na kutumia ubunifu na teknolojia katika kuhakikisha kila mteja anafurahia huduma bora zaidi kila siku", amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda, Mhandisi Richard Swai, ameeleza kwa kina namna ambavyo TANESCO inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wateja katika maendeleo ya shirika na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mafanikio ya TANESCO hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu na wateja, na akawahakikishia kuwa shirika litaendelea kuwa mshirika wa kuaminika katika safari ya maendeleo ya nchi kupitia upatikanaji wa nishati endelevu.

Katika kikao hicho, wateja wamepata fursa ya kuelimishwa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma za TANESCO, ikiwemo miradi mikubwa inayoendelea katika Mkoa wa Shinyanga na hali ya upatikanaji wa umeme.

Elimu imetolewa juu ya Power Factor na umuhimu wake kwa wateja wakubwa, usomaji sahihi wa bili za umeme, na umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kama njia ya kulinda mazingira na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Elimu hii ni sehemu ya dhamira ya TANESCO ya kuhakikisha kila mteja anapata uelewa sahihi kuhusu huduma zake, ili kuimarisha uwazi, uelewa, na ufanisi wa matumizi ya umeme.

Zawadi kwa Wateja

Kama ishara ya kutambua mchango na uaminifu wa wateja, TANESCO ilitoa zawadi mbalimbali, zikiwemo vyeti vya kutambua mchango, saa za ukutani kwa wateja wanaolipa bili kwa wakati, na pressure cooker kwa washiriki waliotoa majibu sahihi kuhusu huduma za TANESCO.

Tukio hili limeleta hamasa na kujenga moyo wa kuthamini huduma bora, uadilifu na uwajibikaji kati ya TANESCO na wateja wake
Ziara ya Kitaaluma

Wateja wamepata pia fursa ya kufanya ziara ya kujifunza katika mradi wa uzalishaji wa umeme wa jua uliopo Wilaya ya Kishapu.

Ziara hii imewawezesha wadau kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa nishati jadidifu na kuelewa namna unavyosaidia kuongeza upatikanaji wa umeme safi na endelevu mkoani Shinyanga.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com