Na Mwandishi wetu, Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbeth Sendiga, ameonya vikali watu au makundi yoyote yanayopanga kufanya vurugu na fujo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kuvuruga amani siku hiyo muhimu kwa taifa.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 21, 2025, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Babati, Mhe. Sendiga amesema kuwa maandalizi ya kiserikali kuelekea uchaguzi huo yamekamilika, huku akihakikisha wananchi wa Manyara kuwa usalama, utulivu na amani vitakuwepo kuanzia kipindi cha kampeni, siku ya kupiga kura, hadi baada ya kumalizika kwa mchakato mzima wa uchaguzi.
“Kama Serikali tunawajibu wa kukemea mapema. Yeyote au kundi lolote linalopanga kufanya vurugu kwa kujishawishi au kushawishiwa, tunatoa onyo kali. Hatutamwacha salama na hatutamvumilia. Amua mapema kama unakuja kupiga kura kwa amani au unataka tukutane mtaani,” amesema kwa msisitizo RC Sendiga.
Amefafanua kuwa Mkoa wa Manyara ni “wrong number” kwa yeyote atakayethubutu kujaribu kuvuruga siku hiyo ya amani, akieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanatekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura bila hofu wala vurugu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akiwataka kurejea majumbani mwao mara baada ya kumaliza zoezi la kupiga kura badala ya kusalia vituoni, jambo ambalo limekuwa likishawishiwa na baadhi ya vyama vya siasa kinyume na miongozo ya Tume ya Uchaguzi.
“Wananchi wakishapiga kura warejee majumbani kuendelea na shughuli zao. Kusalia vituoni siyo sehemu ya miongozo ya uchaguzi, bali ni kinyume cha sheria. Serikali inataka amani, na amani hiyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuilinda,” amesema Mhe. Sendiga.
Kauli ya RC Sendiga imekuja wakati taifa likijiandaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi watapiga kura kuchagua viongozi watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.




Social Plugin