Na Barnabas Kisengi, Dodoma
Aliyekuwa mtia nia nafasi ya ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, Samweli Malecela, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wa Kata ya Mkonze hususan katika mitaa ya Zinje, Mungano ‘B’ na Chinyika kujipanga kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Amesema ni muhimu wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kwa amani na kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi zote,akiwemo Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Paskali Chinyere, pamoja na Madiwani wote wa chama hicho, ili kuendeleza juhudi za maendeleo kwa miaka mitano ijayo (2025–2030).
Akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye mitaa hiyo mitatu, Malecela alieleza kuwa licha ya yeye kutia nia ya kugombea ubunge katika Jimbo hilo, aliheshimu maamuzi ya vikao halali vya chama vilivyompitisha Mhe. Paskali Chinyere kuwa mgombea rasmi wa CCM.
“Mimi kama Samweli Malecela nilitia nia kugombea ubunge wa Dodoma Mjini, lakini chama chetu kina utaratibu wake wa vikao na taratibu,
Tulikuwa wagombea wengi, na chama kilihitaji kumpata mtu mmoja tu,ndiyo maana tukampata Mhe. Paskali Chinyere, ambaye sasa anapeperusha bendera ya CCM. Ni jukumu letu Oktoba 29 kuhakikisha anapata kura za kutosha ili aende Bungeni kuwatumikia wananchi wa Dodoma,” alisema Malecela.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuchagua “mafiga matatu”yaani Rais, Mbunge, na Diwani—wote kutoka Chama Cha Mapinduzi, ili kuhakikisha utekelezaji wa sera na ilani ya chama unakwenda kwa ufanisi bila vikwazo.
Akiendelea kuhamasisha wananchi, Mhe. Malecela aliwataka kutochukulia poa uchaguzi au kususia kupiga kura, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kujinyima haki yao ya msingi ya kikatiba.
“Kauli mbiu yangu ni ‘Oktoba 29 tunatoka kwenda kutiki tiki tatu tu Rais, Mbunge na Diwani wa CCM.’ Wapuuzeni wanaosema msijitokeze. Badala yake, jitokezeni kwa wingi kupiga kura na kuhakikisha ushindi wa chama chetu,” alihimiza.
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya siku ya uchaguzi, kampeni za CCM katika Jimbo la Dodoma Mjini zimeendelea kupamba moto mtaa kwa mtaa na nyumba kwa nyumba, zikilenga kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo Oktoba 29, 2025.


Social Plugin