Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKALA AWAPONGEZA WAZEE WA KIMASAI KWA KUHAMA



Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amezindua rasmi msimu wa sherehe za mila za Kimasai maarufu kama Enkipaata, akiwashukuru wazee wa mila na jamii kwa uamuzi wa kusitisha shughuli za tohara Oktoba 29, 2025, ili kutoa fursa kwa vijana kushiriki upigaji kura wa uchaguzi mkuu.

Sherehe hizo zilizofanyika katika kijiji cha Oldonyosapuk, Wilaya ya Arumeru, zinatarajiwa kuhusisha zaidi ya vijana 2,000 wa kundi rika la Irmegoliki, ambao watahitimisha desturi hiyo ifikapo Oktoba 2032.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Makalla alisema jamii ya Kimasai imeonesha uzalendo na uelewa mkubwa kwa kuzingatia ratiba za serikali na kutambua umuhimu wa kushiriki katika maamuzi ya kitaifa kupitia sanduku la kura.

“Ninawashukuru kwa kunipa heshima hii, na zaidi kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuheshimu taratibu za serikali,tarehe 29 tuungane wote kupiga kura kwa amani, kwani serikali inahakikisha usalama na utulivu katika maeneo yote,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Kimasai, Isack Meijo Ole Kisongo, pamoja na mlezi wa kundi rika hilo, walisema jamii yao imeamua kuipa heshima siku ya uchaguzi kutokana na kutambua umuhimu wa kuchagua viongozi wanaoleta maendeleo.

Wakizungumza kwa niaba ya wazee wa mila, walisema jamii ya Kimasai itaendelea kuwa kinara wa amani na mshikamano, huku wakiahidi kumuunga mkono Mgombea wa Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya katika sekta za ufugaji, elimu, afya na huduma za kijamii.

Sherehe hizo za Enkipaata zimekuwa tukio muhimu la kitamaduni kwa jamii ya Kimasai, zikilenga kuandaa vijana kuwa watu wazima na kuimarisha umoja wa kijamii huku zikiheshimu sheria na taratibu za nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com