Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMANDA MULIRO: TUMEJIPANGA OKTOBA 29, WANANCHI TIMIZENI WAJIBU WENU KIKATIBA




Na Mwandishi wetu, DAR

Jeshi la Polisi nchini limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama na amani vinaendelea kutawala katika kipindi chote cha kuelekea na wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2025 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema jeshi hilo linaendelea kufuatilia kwa umakini matukio yote yanayoweza kuhatarisha amani, huku likizuia na kutanzua mapema vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria.

“Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha wananchi wote wanashiriki uchaguzi mkuu kwa amani,tunafuatilia kwa kina, kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu,” amesema Kamanda Muliro.

Ametoa wito kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kujitoa kwa wingi kushiriki uchaguzi huo ili kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba bila hofu yoyote.

“Tunaomba wananchi waende vituoni kwa utulivu. Vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake bila wasiwasi,” ameongeza.

Kamanda Muliro pia amewataka wanasiasa, wafuasi na wadau wa uchaguzi kuendelea kuhubiri amani na kuepuka kauli au matendo yanayoweza kuibua taharuki katika jamii, akisisitiza kuwa usalama ni jukumu la pamoja.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Watanzania watapiga kura kuwachagua viongozi mbalimbali wa serikali katika ngazi tofauti, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kutoa hakikisho la kuwepo kwa amani, utulivu na haki nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com