Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya James Mgego akiwa ameshika kadi ya chama cha wananchi - CUF baada ya mwanachama huyo kurejesha fomu hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni katika kata ya Ndilimalitembo jimbo la Songea mjini Na Regina Ndumbaro Ndilimalitembo-Songea
Katika hali iliyoonyesha mshikamano na imani mpya kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kada mmoja wa zamani wa Chama cha Wananchi CUF amerudisha rasmi kadi yake na kujiunga na CCM katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya Ndilimalitembo, wilayani Songea.
Tukio hilo limefanyika leo Oktoba 8, mbele ya viongozi mbalimbali wa chama na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Baada ya kurejesha kadi ya CUF, kijana huyo ameomba kupokelewa kama mtoto aliyerejea nyumbani, akiomba msamaha na kuwaomba wana CCM wampe nafasi mpya ya kushiriki katika kuleta maendeleo ya kata hiyo kupitia chama cha mapinduzi.
Mgombea wa udiwani kata ya Ndilimalitembo kupitia CCM, Charles Mhagama (maarufu kama Charles Kabila), amemkaribisha rasmi kwa kumpa tisheti na kofia ya chama, ishara ya kumpokea katika familia ya CCM.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea, James Dan Mgego, amesisitiza kuwa hatua ya kijana huyo kurejea CCM ni ya busara kwani huko alikokuwa hakukuwa na mwanga wa kisiasa.
Ameongeza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye dira ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
"Uchaguzi upo, imani ipo, twende tukapige kura tukichagua CCM, tumechagua maendeleo na amani," amesema Mgego huku akiwahimiza wananchi wa Ndilimalitembo kufanya kata hiyo kuwa mfano kwa kutoa kura nyingi kwa wagombea wa CCM.
Katika hatua nyingine, Mgego amemkabidhi rasmi Charles Mhagama ilani ya CCM kwa ajili ya kuitekeleza mara baada ya kuchaguliwa.
Mhagama, kwa upande wake, amewaomba wananchi wampe kura tatu – ya Rais, Mbunge, na Diwani – zote kwa CCM.
Ameahidi kuwa na uwezo na imani ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa na kutekeleza kikamilifu ahadi zilizopo kwenye ilani ya chama hicho.
Uzinduzi huo wa kampeni umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama ngazi ya kata, wilaya, pamoja na viongozi wa zamani wa udiwani.
Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono mgombea wao huku wakionesha hamasa ya kisiasa na matumaini ya maendeleo kupitia CCM.



Social Plugin