Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JWTZ NA POLISI MOROGORO WAFANYA MAZOEZI YA PAMOJA KUJIIMARISHA KATIKA ULINZI NA USALAMA



Na Mwandishi wetu, Morogoro

Majeshi ya Ulinzi na Usalama mkoani Morogoro, Oktoba 18, 2025, yalifanya mazoezi ya pamoja yenye lengo la kuimarisha mshikamano, ushirikiano na utayari wa kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Mazoezi hayo ambayo yalihusisha askari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi, yameelezwa kuwa ni sehemu ya maandalizi ya kawaida yanayolenga kuongeza ufanisi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na kuwaweka askari katika hali ya utayari wakati wote.

Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, alisema shughuli hiyo haipaswi kutafsiriwa vibaya kama kitisho kwa wananchi, bali ni sehemu ya mpango wa mazoezi endelevu yanayolenga kuboresha uwezo wa pamoja katika kudhibiti matukio ya kihalifu na kuhakikisha amani inatawala.

“Ni muhimu wananchi kuelewa kuwa mazoezi haya ni ya kawaida na yanatoa fursa kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kujipima, kujifunza na kuongeza ufanisi katika kazi zao. Hii ni ishara ya utayari wetu kukabiliana na changamoto zozote za kiusalama, hususan kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu,” alisema SACP Mkama.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki kutoka majeshi mengine walisema mazoezi hayo pia yamekuwa chachu ya kujenga afya ya miili yao, kukuza mshikamano miongoni mwa vikosi mbalimbali, na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mazoezi ya aina hii yamekuwa yakifanyika mara kwa mara katika mikoa mbalimbali nchini, kama sehemu ya jitihada za Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi salama na yenye utulivu wakati wote.





















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com