Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. PHILIP MPANGO ASHIRIKI KILELE CHA JUBILEI YA MIAKA 50 YA KKKT DAYOSISI YA PARE, AZINDUA MNARA WA KUMBUKUMBU



Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo Oktoba 19, 2025, ameshiriki Ibada Maalum ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya kuzaliwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, katika Makao Makuu ya Dayosisi hiyo, Same mkoani Kilimanjaro.

Katika maadhimisho hayo, Dkt. Mpango akiwa pamoja na Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dkt. Alex Malasusa, walizindua mnara wa kumbukumbu wa Jubilei hiyo kama ishara ya shukrani na ukumbusho wa safari ndefu ya huduma ya kiroho na maendeleo iliyoletwa na kanisa hilo kwa jamii kwa kipindi cha nusu karne.

Akizungumza katika tukio hilo, Dkt. Mpango aliipongeza KKKT Dayosisi ya Pare kwa mchango wake mkubwa katika kukuza elimu, afya, amani, na malezi ya kiroho nchini, akisisitiza kuwa kanisa limeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kukuza ustawi wa wananchi.


“Kanisa limekuwa nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye maadili, amani na maendeleo. Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaimarika zaidi,” amesema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Askofu Dkt. Malasusa ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuthamini mchango wa taasisi za dini, na kusisitiza kuwa KKKT itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhubiri amani na kuimarisha ustawi wa jamii.

Jubilei hiyo imehudhuriwa na maelfu ya waumini, viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, na wageni waalikwa, ikiwa ni tukio la kihistoria linaloashiria miaka 50 ya imani, huduma na maendeleo ya Dayosisi ya Pare tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com