Mgombea nafasi ya Ubunge jimbo la Songea mjini Dkt. Damas Ndumbaro na mgombea nafasi ya Udiwani kata ya Mshangano Benson Sovella wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi na wanachama baada ya kuomba kupiga nao picha ya pamojaNa Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Songea Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Damas Ndumbaro, amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wa Kata ya Mshangano waliojitokeza kwa wingi katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya stendi ya Mshangano.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Ndumbaro amewapongeza wananchi na wanachama wa CCM kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha mshikamano mkubwa, akisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha imani yao kubwa kwa chama cha Mapinduzi CCM.
“Nimefurahishwa sana na mapokezi haya, naomba tupige picha ya pamoja kama kumbukumbu ya siku hii muhimu,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro pia ameahidi kuwa serikali itahakikisha barabara ya kutoka Lindi, Mtwara, Tunduru, Namtumbo zitapita katika barabara ya Mshangano kwasababu tunakwenda kuboresha kwa kiwango cha lami.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utachochea maendeleo makubwa katika eneo hilo na kuifanya Mshangano kuwa “downtown” ya Songea kutokana na shughuli nyingi za kimaendeleo zitakazojitokeza.
Kwa upande wake, mgombea wa Udiwani wa Kata ya Mshangano kupitia CCM, Benson Sovella, amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha ushirikiano mkubwa katika kampeni hizo.
Sovella amesema amekabidhiwa mkataba wa ilani ya CCM kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, akibainisha kuwa mambo mengi yaliyomo katika ilani hiyo ni ya kimaendeleo na yataletwa Mshangano.
Amesisitiza kuwa kata hiyo ni miongoni mwa kata chache zitakazopata kituo cha afya chenye ubora na viwango vya juu katika Manispaa ya Songea.
Sovella pia amewaomba wananchi kumpa kura ya ndio pamoja na wagombea wengine wa CCM, akiwahimiza kuwa maendeleo yanapatikana kupitia ushirikiano wa viongozi watatu wa chama hicho – Rais, Mbunge, na Diwani.
“Ugali hauwezi kuiva bila mafiga matatu tuwape kura viongozi wetu wa CCM ili tuendelee kuleta maendeleo,” amesema Sovella, akiahidi kutowaangusha wananchi wa Mshangano endapo atapewa ridhaa.
Meneja wa Kampeni wa Wilaya ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya, Mandwanga Banda, amewahakikishia wananchi kuwa kero mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo vivuko, maji na miundombinu ya eneo la TBC, zipo mbioni kupatiwa suluhisho.
Amesema serikali imetenga shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya mradi wa maji katika maeneo ya Mitendewawa na Songea Mjini kwa ujumla na mkandarasi tayari yupo kazini.
Aidha, amebainisha kuwa ndani ya miezi sita ijayo, eneo la TBC litajengwa studio ya kisasa ya kanda ya kusini pamoja na ofisi kubwa na nyumba za watumishi, akiwataka wananchi kuwa wavumilivu kwani mambo mazuri yanakuja.



Social Plugin