
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kimehitimisha kampeni zake kwa kishindo katika kata ya Bombambili, jimbo la Songea Mjini, mkoani Ruvuma, ambapo mamia ya wananchi wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono chama hicho.
Mgeni rasmi katika mkutano huo ni Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Ahmed khalfani , ambaye amesisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma waeendelee kuiamini CCM kutokana na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za maendeleo unaofanywa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mkutano huo, Ahmed khalfani amesema wananchi wa Songea hawapaswi kuwa na mashaka, tukahakikishe CCM inashinda kwa kishindo katika majimbo yote tisa ya mkoa huo pamoja na kata zote 173.
Amesema mafanikio makubwa yameonekana katika sekta za miundombinu ya barabara elimu, na afya, akitaja mabadiliko kama kuanzishwa kwa safari tatu za ndege kwa wiki mkoani Ruvuma, elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari, na mpango wa serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya.
Ameongeza kuwa serikali ya Rais Samia itaendelea kuboresha huduma za afya, ikiwemo kuhakikisha ndugu wanaopoteza maisha hospitalini wanatolewa bure bila kudaiwa fedha, pamoja na kuendeleza ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji.
Aidha, amewataka madiwani wa CCM kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ya Manispaa zinawanufaisha walemavu, wanawake, vijana na wazee, kama inavyoelekezwa kwenye sera za chama hicho.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Songea Mjini, Dkt. Damasi Ndumbaro, amesema kampeni zao za siku 60 zimefanyika kwa mafanikio makubwa na wananchi wameona matokeo ya kazi za maendeleo zinazotekelezwa na serikali ya CCM.
Ametaja miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, masoko ya Manzese A na B, shule ya msingi Ruvuma, na chuo kikuu kipya cha Songea kuwa ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani ya CCM.
Dkt. Ndumbaro amewaaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura, akisisitiza kuwa kuipa kura CCM ni kuchagua maendeleo endelevu na mustakabali bora wa Songea.


Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Ahmed khalfani
Social Plugin