Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BODABODA NA MACHINGA: HATUTAKUWA CHANZO CHA KUVUNJA AMANI YETU



Na Mwandishi wetu, DAR

Makundi ya waendesha bodaboda na wamachinga yamejitokeza kwa wingi jijini Dar es Salaam katika matembezi ya amani yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Posta, Kisutu, Kivukoni, Kariakoo, Karume na Buguruni, yakiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kulinda amani na kushiriki kwa utulivu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa matembezi hayo, Kiongozi wa waendesha bodaboda Wilaya ya Ilala, Abdul Kimaro, aliwataka vijana wenzake kuepuka kurubuniwa na watu wanaotaka kuvuruga amani, badala yake wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amani.

Kimaro alisema kundi la bodaboda limeamua kuwa sehemu ya ulinzi wa amani kwa sababu amani ni msingi wa maendeleo na chanzo cha mafanikio yao binafsi na kijamii. Aliongeza kuwa vurugu na migogoro haina manufaa kwa wananchi, bali huathiri shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wao, makundi ya wamachinga na wajasiriamali wadogo wakiwemo mama na baba lishe walionesha kukubali elimu hiyo na kuahidi kujitokeza kupiga kura kwa amani. Walisema kuwa uchaguzi ni fursa ya kuchagua viongozi bora, siyo uwanja wa kugombana au kuharibu mali.

Wamachinga hao walisema kuwa wameamua kushiriki kampeni ya amani kwa sababu wao ni sehemu kubwa ya jamii na wanatambua umuhimu wa utulivu katika kipindi cha uchaguzi.

Viongozi wa makundi hayo wamesisitiza kuwa uchaguzi ni fursa ya maendeleo na siyo sababu ya migogoro, na kwamba wataendelea kuwa mstari wa mbele kuhimiza vijana wenzao kulinda amani katika kipindi chote cha uchaguzi hadi baada ya kutangazwa kwa matokeo.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com