Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NI DARAJA LA HAKI, TUITUNZE KWA GHARAMA YOYOTE : ASKOFU DKT. WILLY AKYOO




Na Mwandishi wetu, Arusha 

 Askofu Mkuu na Muasisi wa Makanisa ya Bethel Calvary nchini Tanzania, Baba Askofu Dkt. Willy Akyoo, amesema amani ni daraja la haki katika jamii, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda kwa gharama yoyote kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Meru, mkoani Arusha, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Askofu Akyoo amesema bila amani, hakuna haki, maendeleo, wala maelewano yanayoweza kupatikana katika jamii.

“Umuhimu wa amani kwa Tanzania umekuwa mjadala mkubwa,Wapo wanaosema hakuna amani bila haki, lakini mimi naamini amani ndiyo daraja la kwenda kwenye haki. Amani ikiwepo, ndipo haki inaweza kupatikana kwa njia sahihi. Huwezi kupata haki kama hakuna amani, kwa sababu hata anayeshikilia haki yako huwezi kuzungumza naye bila utulivu,” amesema Askofu Dkt. Akyoo.

Askofu Akyoo ameeleza kuwa amani huwezesha mifumo ya kisheria na kijamii kufanya kazi ipasavyo, hivyo kutoa mazingira mazuri ya haki na huduma bora kwa wananchi. Amesisitiza kuwa bila amani, jamii hupoteza misingi yake ya maelewano na ustawi.

Aidha, amerejea mafundisho ya vitabu vitakatifu, akisema maandiko yanatoa maagizo kwa waumini “kuitafuta amani kwa bidii na kwa watu wote”, akisisitiza kuwa wajibu wa kulinda amani ni wa kila mmoja bila kujali itikadi au nafasi aliyonayo.

Akitoa wito kwa vijana, Askofu Akyoo amewaonya dhidi ya kutumika katika vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu au propaganda za kisiasa zinazoweza kuhatarisha utulivu wa taifa.

“Vijana wasikubali kutumika kuratibu ama kushiriki matendo yanayovunja amani. Wana jukumu la kulinda hatma zao na mustakabali wa nchi yao,” amesema.

Amesisitiza pia umuhimu wa vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisema hatua hiyo ndiyo mwanzo wa wao kuamua hatma ya taifa na kujenga Tanzania yenye haki, maendeleo na amani endelevu.

“Kupiga kura ni mwanzo wa vijana kuitawala nchi yao. Ni nafasi ya kuchagua viongozi watakaolinda amani na mustakabali wa vizazi vijavyo,” ameongeza Askofu Akyoo

Askofu Dkt. Akyoo amehitimisha kwa kuwataka Watanzania wote kuendelea kuienzi amani kama urithi na nguzo kuu ya taifa, akisisitiza kuwa bila amani, hakuna haki, na bila haki, hakuna maendeleo.

“Amani ni urithi tuliopewa na Mungu. Ni jukumu letu sote kuilinda, kuithamini na kuienzi kwa gharama yoyote ile,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com