Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na mwanasiasa mashuhuri barani Afrika, Raila Amollo Odinga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa kutoka kwa familia na vyanzo vya hospitali zimethibitisha kuwa Odinga alifariki leo alfajiri nchini India, ambako alikuwa akipokea matibabu.
Msemaji wa kituo hicho ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Odinga alilalamika kwa matatizo ya kupumua kabla ya kuzimia saa 1:45 asubuhi.
Alikimbizwa katika hospitali ya karibu ya kibinafsi, lakini juhudi za madaktari hazikuweza kuokoa maisha yake.
Maisha na Safari ya Kisiasa ya Raila Odinga
Raila Odinga alizaliwa Januari 7, 1945, akiwa mwana wa Jaramogi Oginga Odinga, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya baada ya uhuru.
Alisomea Ujerumani Mashariki katika fani ya uhandisi kabla ya kurejea Kenya mwishoni mwa miaka ya 1970.
Katika kipindi cha uhai wake, Raila alihusishwa sana na harakati za kupigania demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Aliwekwa kizuizini kwa zaidi ya miaka sita kufuatia tuhuma za kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka 1982 dhidi ya serikali ya Rais Daniel Arap Moi.
Baada ya kuachiliwa na kurejea kutoka uhamishoni, alichangia kwa kiasi kikubwa katika harakati za kuleta mfumo wa vyama vingi nchini Kenya. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioongoza kuking’oa chama tawala cha KANU mamlakani mwaka 2002 kwa kumuunga mkono Rais wa zamani, Mwai Kibaki.
Uongozi na Urithi wa Kisiasa
Raila Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya kati ya mwaka 2008 hadi 2013, kupitia makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kufuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007.
Aligombea Urais mara tano (1997, 2007, 2013, 2017 na 2022), lakini hakuwahi kupata wadhifa huo licha ya kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya.
Raila, maarufu kwa jina la "Baba", ataendelea kukumbukwa kama nguzo muhimu ya demokrasia ya Kenya na Afrika, mpigania haki na kiongozi aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya mageuzi ya kisiasa na kijamii.
Maisha Binafsi
Raila Odinga ameacha mjane, Mama Ida Odinga, na watoto wanne, akiwemo Raila Junior. Alikuwa mtu wa familia, mpenzi wa michezo, hususan soka, na mara kadhaa alionekana kuunga mkono timu za nyumbani katika mashindano mbalimbali.
Pole na Rambirambi
Viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wameanza kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya Raila Odinga na wananchi wa Kenya, wakimtaja kama "shujaa wa demokrasia", "nguzo ya siasa za upinzani", na "kiongozi aliyewatetea wanyonge".
Tutaendelea kukujuza taarifa zaidi kuhusu mipango ya mazishi na maombolezo kadri zinavyotolewa.
Social Plugin