Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHOMVU: COP30 NI FURSA KUINUA SAUTI ZA TANZANIA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI

Meneja Uendeshaji kutoka CAN, Boniventure Mchomvu.

Na Kadama Malunde - Morogoro

Meneja Uendeshaji kutoka Shirika lisilo la kiserikali Climate Action Network Tanzania (CAN), Boniventure Mchomvu, amesema Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Novemba 10–21, 2025 mjini Belem, Brazil ni jukwaa muhimu kwa Tanzania kupanua ajenda zake za kitaifa na kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika kikao kazi cha kujengea uwezo waandishi wa habari kilichofanyika Oktoba 22–24, 2025 mkoani Morogoro, Mchomvu alisema mkutano wa COP30 unatoa nafasi kwa Tanzania kufuatilia utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika mikutano ya awali na kuwasilisha vipaumbele vipya, hususan katika maeneo ya fedha za tabianchi, teknolojia rafiki kwa mazingira, na utafiti wa kisayansi unaolenga kuongeza uthabiti wa jamii zilizoathirika.

“Ukiangalia, Tanzania inakwenda na malengo zaidi ya 12 ambayo yanalenga kuishirikisha dunia juu ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya kitaifa. Janga hili halina mipaka ya kisiasa, hivyo ni wajibu wetu kulishughulikia kwa pamoja,” amesema Mchomvu.
“Huu ni wakati wa Tanzania kuongeza sauti yake kimataifa na kuhakikisha ajenda zetu za kitaifa, hususan zinazohusu usawa wa kijinsia, nishati safi na uhimilivu wa jamii, zinapata nafasi mezani kwenye majadiliano ya dunia,” ameongeza Mchomvu.

Mchomvu ameeleza kuwa, mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamelenga kuongeza uelewa na uwezo wa kuandaa habari zenye maudhui ya mabadiliko ya tabianchi kabla, wakati, na baada ya mkutano wa COP30, ili Watanzania waweze kufahamu fursa na wajibu wa taifa katika mapambano haya ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dastan Kamanzi, amesema kikao kazi hicho kimeandaliwa na TMF kwa kushirikiana na Oxford Policy Management (OPM) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uingereza na Uswisi, huku CAN Tanzania ikitoa utaalamu na uzoefu katika masuala ya tabianchi na maandalizi ya COP30.
Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi akizungumza.

“Mradi huu wa miezi minne unalenga kuzalisha habari zenye maudhui ya mabadiliko ya tabianchi. Tunataka waandishi waandike habari zenye tija na ubora, zitakazoendana na mijadala itakayojitokeza wakati wa COP30 na baada yake. Tunaanza kuandika mapema, kabla ya mkutano, ili Watanzania waelewe nini kinaendelea,” amesema Kamanzi.

Kikao kazi hicho kimeshirikisha waandishi 20 kutoka mikoa 13 ya Tanzania kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, redio na magazeti.
Nurturer - Bakari Khalid

Walezi wa waandishi (nurturers), akiwemo Sammy Awami, Rashidi Kejo, Sanura Athanas, Bakari Khalid na Said Mmanga, wamesisitiza kuwa waandishi wa habari wanayo nafasi muhimu katika kuongeza uelewa wa jamii na kuwawajibisha watendaji wa serikali kuhusu utekelezaji wa sera za tabianchi.

Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho, akiwemo Hadija Omary Mazezele, Arodia Peter na Denis Sinkonde, wamesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kuandaa habari bora, zenye uchambuzi wa kina na mtazamo wa kitaifa kuhusu ajenda za COP30.
Mkutano wa COP (Conference of the Parties) ni jukwaa kuu la kimataifa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC). Kila mwaka, COP hukusanya viongozi wa serikali, wataalamu, wanahabari, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kujadili hatua za pamoja za kupunguza hewa chafuzi, kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuimarisha ushirikiano wa kifedha na kiteknolojia.

Mkutano wa mwisho, COP29, ulifanyika mwaka 2024 mjini Baku, Azerbaijan, na ulijikita katika mjadala wa fedha za tabianchi na utekelezaji wa ahadi za kupunguza gesi ukaa.

Kwa Tanzania, COP30 ni fursa adhimu ya kuongeza ushiriki wake kimataifa katika maamuzi ya tabianchi, kuwasilisha mafanikio ya kitaifa kama miradi ya nishati jadidifu, uhifadhi wa misitu, na mikakati ya kijinsia katika mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kujifunza mbinu mpya kutoka kwa mataifa mengine.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com