Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TASAC YATOA ELIMU YA USALAMA KWA WAMILIKI WA MABOTI MATEMA


Mfawidhi wa TASAC Wilayani Kyela Naho. David Chiragi akiongea
katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika ufukweni mwa ziwa hilo

Na Woinde Shizza ,Mbeya

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini limeendesha kampeni ya kutoa elimu kwa wamiliki wa boti, wafanyabiashara na wapakia mizigo katika kijiji cha Matema, wilayani Kyela, mkoani Mbeya.

Elimu hiyo imelenga kuimarisha usalama wa usafiri wa usafiri majini katika Ziwa Nyasa, kwa lengo la kupunguza ajali na kulinda maisha ya wananchi wanaotegemea usafiri huo kwa biashara na shughuli zao za kila siku.

Akizungumza katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika ufukweni mwa ziwa hilo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Wilayani Kyela Naho. David Chiragi aliwataka wamiliki wa vyombo vidogo vya usairi majini kuhakikisha wanazingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.
“Mojawapo ya kanuni muhimu ni kuzuia safari za usiku, Safari zianze saa 12 asubuhi na kumalizika jioni ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea gizani na kila abiria anatakiwa kuvaa jaketi okozi muda wote wa safari,” alisema huku akisisitiza kuwa katika usafiri majini hakuna ajali za bahati mbaya, bali ni uzembe na kutozingatia kanuni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Bandari ya Matema, Beat Andrew Haule, aliwataka madereva na wamiliki wa maboti kuhakikisha wanatimiza masharti yote yaliyowekwa na TASAC ili kufanya kazi kwa usalama na ufanisi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Maboti Wilaya ya Kyela, Macarus Gowele, alisema wao kama wamiliki wamekuwa wakifanya kazi zao kutoka eneo la Matema, wakipita Kapinga kuelekea Ludewa,ambapo alisema hata hivyo, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika safari hizo.
“Tunapokuwa safarini mara nyingi tunakosa huduma za msingi kama vyoo na sehemu za kulala endapo tunakwama njiani, hasa wakati wa mvua ,tunaomba serikali itupatie huduma hizo katika baadhi ya vituo ili tupate msaada tunapokutana na changamoto,” alisema Gowele.

Wananchi na wamiliki wa maboti walioshiriki kikao hicho waliipongeza TASAC kwa kutoa elimu hiyo, wakisema itasaidia kuimarisha usalama wa abiria na mizigo, kukuza biashara na kuendeleza shughuli za utalii katika eneo la Matema Beach.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com