Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JENISTA MHAGAMA: "LITAPWASI BILA KUPIGA KURA NI KUPOTEZA MAENDELEO"


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jenista Mhagama akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Uyahudini Kata ya Litapwasi Jimbo la Peramiho Septemba 28,2025

Na Regina Ndumbaro-Litapwasi

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jenista Mhagama, ameendelea na kampeni zake kwa kutembelea Vijiji vitatu vilivyopo katika Kata ya Litapwasi, Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini, ambapo amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Uyahudini.

Katika mkutano huo uliofanyika Septemba 28,2025, Mhagama amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba, akisisitiza kuwa hiyo ni siku muhimu ya kuamua maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimsingi kwa wananchi wa Litapwasi.

Amesema, “Litapwasi itakuwa imepoteza muda ikiwa haitatumia haki yake ya kupiga kura.”

Katika hotuba yake, Mhagama amemtambulisha mgombea udiwani wa CCM kwa Kata ya Litapwasi, Ndugu Rajabu Mtiula, maarufu kama "Rajabu Buldoza", akimwelezea kuwa ni kiongozi mwenye uwezo na aliyeaminiwa na wananchi.

Ameeleza kuwa CCM haikuweka mgombea mwingine wa Udiwani katika Kata hiyo kwa kuwa walimwamini Rajabu anatosha katika nafasi hiyo.

Aidha, amebainisha kuwa yeye ni mgombea pekee wa Ubunge katika Jimbo la Peramiho baada ya kukosekana kwa mpinzani yeyote, hivyo akawataka wananchi kuhakikisha wanakamilisha “mafiga matatu” kwa kumchagua Rais, Mbunge na Diwani wote kupitia CCM.

Mhagama ameahidi miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa ofisi ya Kijiji cha Uyahudini, madarasa, vyoo, taa za barabarani, umeme katika vitongoji vyote, maji safi, na kuletwa kwa Watumishi wa zahanati ya Kijiji hicho.

Ameeleza kuwa serikali ya CCM kupitia ilani yake imejipanga kutoa mikopo kwa wananchi, kujenga ofisi za ununuzi wa mahindi, pamoja na kuleta mashine za kukamua alizeti ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wa eneo hilo.

Jenista Mhagama amewaomba wananchi wa Litapwasi kutoa kura za kutosha kwa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi zote tatu, akisisitiza kuwa CCM ndio chombo pekee chenye dira ya kweli ya maendeleo kwa wananchi wa vijijini.

Amesisitiza kuwa ushiriki wao kwenye uchaguzi huo ni msingi wa mabadiliko na mafanikio ya muda mrefu katika jamii yao.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com