Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

COASCO YATOA MAFUNZO KWA VIONGOZI NA WATENDAJI WA VYAMA VYA USHIRIKA NCHINI

Na Mwandishi wetu Malunde 1 Blog. 

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limehitimisha mafunzo maalum ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu Agosti 26 hadi 28, 2025 jijini Dodoma.

Mafunzo hayo yaliyolenga kuimarisha uongozi, uwajibikaji na utendaji bora ndani ya sekta ya ushirika, yamewajumuisha pia wahasibu wa vyama, ambao walipata fursa ya kujifunza kuhusu mabadiliko mapya ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 pamoja na sheria mbalimbali za kodi zinazogusa shughuli za vyama vya ushirika nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, CPA Golden Kajaba, mmoja wa wakufunzi wakuu wa COASCO, amesema kuwa mabadiliko ya hivi karibuni kwenye sheria za fedha na kodi yanaleta athari kubwa katika namna vyama vya ushirika vinavyoendesha shughuli zake za kila siku.

“Ni muhimu kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kuelewa athari za mabadiliko haya ya kisheria, ili waweze kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyama, na kulinda maslahi ya wanachama,” amesema CPA Kajaba.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuongeza uwazi, kuimarisha imani ya wanachama kwa vyama vyao, na kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa nguzo thabiti ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.

Mafunzo hayo yamepata mwitikio mkubwa na yameelezwa kuwa ni chachu ya mageuzi katika mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa vyama vya ushirika, hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com