
Na Hadija Bagasha -Mwanza
Mgombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha wananchi CUF Gombo Samandito Gombo ameahidi kwamba iwapo atapata ridhaa ya kuongoza Watanzania katika Serikali yake atahakikisha kila mwananchi anaingiziwa umeme nyumbani kwake bila malipo yeyote kwa kuwa Tanesco ni shirika la umma ambalo wananchi wanalipa kodi zao.
Mgombea Urais Gombo Samandito ametoa ahadi hiyo akinadi sera ya chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kanyala, Kata ya Bhulyaheke Wilayani Buchosa Mkoani Mwanza.
Awali akizungumza na wananchi hao mgombea Urais Gombo amesema kwamba anasikitika kuona wananchi wanachangia huduma za umeme ambazo kwenye serikali yake atahakikisha anayafuta malipo hayo.
"Suala la umeme hivi sasa wananchi mnalipia ndio muletewe majumbani chama cha wananchi CUF tunasema Tanesco atakapoona nyumba imejengwa imekamilika atakukimbilia atakukimbilia yeye kuja kukuwekea umeme na wewe mwananchi mpaka nyumbani kwako na kukuunganishia huduma hutochangia chochote zaidi ya kujinunulia kavocha mwenyewe", amesisitiza Gombo.
"Tanesco ni shirika la Umma ni shirika la serikali asilimia 100 inawezekanaje mtu uambiwe kulipia milioni moja eti kwasababu nguzo ziko mbali na nyumbani kwako na wakati huo huo kodi umeshalipa na rasilimali zipo miti ipo imejiotea yenyewe tu, "amebainisha Mgombea urais Gombo.
"Sisi CUF tunasema umeme utaingizwa mpaka kwenye nyumba yako bila wewe kuomba wewe utaukuta umeme umeshakufikia unachotakiwa ni kutafuta fundi wa wayaring akafanye wayaring tanesco wakuletee huduma ufuarahie na watoto wako ma mkeo ili muijaze dunia, "amesema Gombo.
Akizungumzia suala la afya hospitalini mgombea urais huyo amesema atahakikisha atakapochaguliwa kila mwananchi anatibiwa bure hospitali zote kwakuwa katika maisha huduma namba moja ni afya.
Gombo Samandito amesema ifikapo mwezi octoba huduma za afya zitatolewa bure kwa kila mtanzania kwakuwa hakuna sababu ya kufanya michango yeyote kwa kuwa nchi ya Tanzania ina rasilimali za kutosha zinazoweza kuendesha na kusimamia huduma za Watanzania.
"Ajira hakuna mahospitalini kuna uaba mkubwa wa watumishi wa afya lakini pia kwenye majeshi ya polisi ni maeneo ambayo yana upungufu mkubwa wa watumishi huku watanzania wengi wenye elimu wakiishia kubaki majumbani bila ajira yeyote kwanini watumishi wawe wachache ili hali tuna rasilimali kubwa ya vijana ambao wamesoma na wapo majumbani?, Alihoji mgombea urais huyo.






Social Plugin