Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAMATWA KWA BIASHARA HARAMU YA NYARA NA BIDHAA BANDIA RUVUMA

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco G Chilya akionesha meno yaliyokamatwa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Hifadhi ya Wanyamapori TAWA 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori TAWA kikosi dhidi ya ujangili Ruvuma Songea (TAWA), limefanikiwa kuwanasa watuhumiwa saba wanaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali, huku wengine wakikamatwa kwa kutengeneza na kusambaza bidhaa bandia. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 21, 2025, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya amesema jumla ya matukio manne makubwa ya kihalifu yameripotiwa katika oparesheni hiyo.

Katika tukio la kwanza, SACP Chilya amesema watuhumiwa saba walikamatwa na nyaraka za serikali pamoja na meno ya tembo 64, yakiwemo meno nane mazima na vipande 56, meno ya kiboko 145 na meno ya ngiri mawili, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 314. 

Meno hayo yalikuwa yamefichwa kichakani na ndani ya mashimo kinyume na sheria za uhifadhi wa wanyamapori.

Tukio jingine linahusisha ukamataji wa watuhumiwa katika kata ya Peramiho kijiji cha Mgazini, Songea Vijijini, na kata ya Shauli Tanga, Manispaa ya Songea, tarehe 18 Agosti 2025. 

Oparesheni hiyo iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya polisi na Jeshi la Hifadhi ya Wanyama pori, inalenga kukomesha uwindaji haramu na biashara ya nyara za serikali katika mkoa wa Ruvuma.

Katika hatua nyingine, polisi walimkamata Maiko Lusekelo Mwakifuna (50), mkazi wa Mjimwema, akiwa anazalisha bidhaa bandia za vinywaji aina mbalimbali ikiwemo Musta Potable, Konyagi, na Smartgin. 

Miongoni mwa vielelezo vilivyokamatwa ni chupa tupu zenye lebo za TRA, kemikali, madumu, stika bandia, na vifaa mbalimbali vya kuzalishia pombe hiyo bila leseni halali.

Kamanda Chilya ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kusaidia kulinda rasilimali za taifa.

 Pia amesisitiza kuwa jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kusimamia usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kuhakikisha uchaguzi wa amani kwa madiwani, wabunge na rais.Chupa ,madumu,maboksi ya konyagi na smartgin na vizibo, stika za TRA zilizokamatwa kwa mfanyabiashara wa pombe bandia zisizothibitishwa na serikali ndugu Maiko Lusekelo Mwakifuna kutoka kata ya Mjimwema Manispaa ya Songea 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com