Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mgombea urais wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis,amechukua fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)huku akiahidi kuwa serikali yake itafanya mageuzi makubwa ya sekta ya afya endapo atachaguliwa kuongoza nchi, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora bila kubebeshwa gharama zinazowakwamisha kupata matibabu.

Akizungumza leo Agosti 15, 2025 jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) akiwa pamoja na mgombea mwenza Balozi Dkt. Evaline Wilbard Munisi,Amber amesema,“Tumeona watu wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma hospitalini na kutoweza kumudu gharama za matibabu,hali hii lazima ikomeshwe,” amesema

Khamis amesisitiza kuwa mpango wa NCCR Mageuzi ni kuwekeza zaidi kwenye rasilimali watu na miundombinu ya afya, sambamba na kuimarisha ustawi wa jamii, ili maendeleo ya taifa yawe na msingi wa afya bora kwa wananchi.

Ikumbukwe kuwa hatua hiyo ya kuchukua fomu imefuata baada ya kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR Mageuzi kilichofanyika jana Agosti 14, 2025 jijini Dodoma, ambapo wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kumteua Balozi Dkt. Munisi kuwa mgombea mwenza wa urais wa Muungano.

Katika kikao hicho, Leila Rajabu Khamis aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 57 kati ya 58 za wajumbe waliohudhuria.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho cha jana pia kiliidhinisha Ilani ya Uchaguzi 2025–2030 yenye vipaumbele 11, ikiwemo kuboresha sekta ya afya na ustawi wa jamii,Kukuza usawa wa kijinsia na kushughulikia mahitaji ya makundi maalum.

Vipaumbele vingine ni Kurejesha maadili ya kitaifa na kuimarisha uadilifu wa viongozi,Kuendeleza sekta za mifugo, madini, maliasili, utalii na Kuimarisha usalama wa taifa.