Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika kuadhimisha Wiki ya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea kitaifa Dodoma, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo nchini kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS).
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa maonesho hayo leo Agosti 1,2025 Dodoma,Afisa Biashara wa Benki hiyo, Rosemary Gordon, amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2018 chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ukiwa na mtaji wa shilingi bilioni 54 kwa lengo la kuwawezesha wakulima wadogo kupata mikopo kwa urahisi zaidi kupitia dhamana inayotolewa kwa taasisi za kifedha zinazowahudumia.
Kwa mujibu wa Rosemary, tangu kuanzishwa kwake, jumla ya taasisi za kifedha 19 zimepatiwa dhamana kupitia mfuko huo, na hadi sasa umenufaisha zaidi ya wakulima wadogo 762,291 kote nchini.
"Mfuko huu ni suluhisho kwa changamoto ya wakulima wadogo kukosa dhamana ya kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao za kilimo na ufugaji," amesema.
Rosemary amefafanua kuwa benki inatoa mikopo kwa mnyororo mzima wa thamani ya kilimo, ikiwemo uzalishaji, usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na masoko. Hii inahusisha kusaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo kama mbegu bora, mbolea, dawa za kudhibiti magonjwa na visumbufu, pamoja na zana za kisasa zikiwemo matrekta, power tillers na vifaa vya uvunaji.
Aidha, amesema mfuko huo haujawaacha wafugaji na wavuvi nyuma kwani pia unatoa dhamana kwao ili waweze kukua kiuchumi na kuongeza tija.
"Tunafanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, tukisisitiza zaidi mikopo kwa wanawake na vijana ili kuhakikisha makundi haya yanawezeshwa," amesema.
Takwimu zilizotolewa na benki zinaonyesha kuwa hadi sasa shilingi bilioni 43.6 zimetolewa kwa dhamana ya mikopo ya wakulima kununua zana za kilimo na vifaa vya kisasa, huku zaidi ya bilioni 197 zikitolewa kama dhamana ya mikopo kwa ajili ya pembejeo.
Kwa upande wake, Mariam Leonard, Afisa Biashara wa TADB Kanda ya Kati, amesema benki hiyo inashiriki maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mikopo ya moja kwa moja inayotolewa na benki kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini.
“Mpaka sasa benki imekwishatoa zaidi ya shilingi trilioni 1.1 kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kote. Tunawakaribisha wakulima kutembelea banda letu hapa kwenye maonesho ya Nanenane ili wapate elimu ya fursa za mikopo na huduma mbalimbali tunazotoa,” amesema Mariam.
Ameongeza kuwa, dhana ya mkulima imepanuka na inahusisha wadau wote wa mnyororo wa thamani – kuanzia wazalishaji wa mazao, wachakataji, wauzaji wa pembejeo, wafanyabiashara wa mazao, wafugaji na wavuvi.
"Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mdau wa kilimo anayeachwa nyuma katika safari ya kuongeza tija na uzalishaji," amesema.
Rosemary amesisitiza kuwa mfuko wa dhamana umekuwa nguzo muhimu ya mapinduzi ya kilimo nchini kwa kusaidia wakulima ambao awali walikuwa wanashindwa kupata mikopo kutokana na kukosa dhamana.
“Mfuko huu ni kielelezo cha dhana ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumuinua mkulima mdogo kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo cha kibiashara,” ameongeza.
Katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa TADB, benki imekuwa mshirika muhimu katika utekelezaji wa sera za kilimo kwa kutoa huduma za kifedha zenye masharti nafuu, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo na taasisi za kifedha nchini.
TADB na Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo wameonyesha njia sahihi ya kuhakikisha mkulima anapata mtaji, teknolojia na elimu, hivyo kubadilisha maisha yake na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa taifa.




Social Plugin